(Mathayo 11:1-14)
“Ikawa Yesu alipokwisha kuwaagiza wanafunzi wake kumi na wawili, alitoka
huko kwenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao. Naye Yohana aliposikia huko
gerezani matendo yake Kristo, alituma wanafunzi wake, kumwuliza, ‘Wewe ndiwe
yule ajaye, au tumtazamie mwingine?’ Yesu akajibu akawaambia, ‘Nendeni mkamweleze
Yohana mnayoyasikia na kuyaona; vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye
ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa
habari njema. Naye heri awaye yote asiyechukizwa nami.’ Na hao walipokwenda
zao, Yesu alianza kuwaambia makutano habari za Yohana, ‘Mlitoka kwenda nyikani
kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na upepo? Lakini mlitoka kwenda kuona nini?
Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Tazama, watu wavaao mavazi mororo wamo katika
nyumba za wafalme. Lakini kwa nini mlitoka? Ni kuona nabii? Naam, nawaambia, na
aliye mkuu zaidi ya nabii. Huyo ndiye aliyeandikiwa haya,
‘Tazama, mimi namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza
njiayako mbele yako.’ Amin, nawaambieni, hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake
aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji; walakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni
ni mkuu kuliko yeye. Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa
mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka. Kwa maana manabii wote
na torati walitabiri mpaka wakati wa Yohana. Na ikiwa mnataka kukubali, yeye
ndiye Eliya atakayekuja.”
Tunapaswa
Kuifahamu Huduma ya Yohana Mbatizaji
Ni huduma gani hasa ambayo Yohana Mbatizaji aliitimiza
kabla ya Yesu? Wakristo wengi leo hii hawamfahamu vizuri Yohana Mbatizaji,
hivyo wanatakiwa kupata mtazamo mpya kuhusu Yohana Mbatizaji ili waweze kumfahamu
na kuikubali huduma yake kikamilifu. Sisi sote tunapaswa kuwa na ufahamu sahihi
na kuukubali uhusiano kati ya huduma ya Yesu na ile yaYohana Mbatizaji. Kwa kuufahamu
uhusiano huu kikamilifu, basi unapaswa kwanza kulipokea ondoleo la dhambi kwa
imani.
Katika kifungu cha leo cha Maandiko, Yesu aliwaambia
wanafunzi wa Yohana Mbatizaji, “Nendeni mkamweleze Yohana mnayoyasikia na kuyaona; vipofu
wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia,
wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema.
Kwa kweli vipofu waliokutana na Yesu walifunguliwa
macho yao, viwete waliweza kusimama na kutembea, waliokuwa wamepagawa na mapepo
waliwekwa huru, na injili ilihubiriwa kwa maskini wa roho.
Tunachopaswa kukitambua hapa ni kwamba huduma ya
Yesu ilihusisha kazi ya kuwafungua macho vipofu. Kwa maneno mengine, katika
wakati huu, Bwana ametupatia injili ya maji na Roho, ambayo ni injili ya kweli
inayowafungua macho wenye dhambi ambao bado wanatembea katika giza. Kabla ya
kukutana na Yesu Kristo, kila mtu alikuwa na dhambi katika moyo wake na alikuwa
ni kipofu wa kiroho mbele ya Mungu. Sisi pia, tulikuwa hatuufahamu uhalisia wa
injili ya maji na Roho, wala hatukutambua kuwa Yesu ni nani, pia sisi sote tulikuwa
hatuzifahamu dhambi zetu na matokeo mabaya ambayo yangejiri kwa sababu ya
dhambi hizo. Pia hatukuwa na upendo kwa Neno la kweli la injili ya maji na Roho,
ambalo ni Kweli ya wokovu ambayo Yesu ametupatia.
Hata hivyo, watu wengi sasa wameisikia Neno lenye
nguvu la injili ya maji na Roho, na kwa kule kuiweka imani yao katika Neno la
injili, basi macho yao ya kiroho yamefunguliwa na wameuvumbua Ukweli unaowawezesha
kuokolewa toka katika dhambi zao zote. Wale wanaoifahamu na kuiamini injili hii
ya kweli sasa wameuvumbua Ukweli wa ondoleo la dhambi ambao walikuwa
hawaufahamu hapo kwanza: Macho yao ya kiimani yamefunguliwa, na sasa wanaifanya
kazi ya Mungu. Kama ilivyo katika macho yetu ya kimwili ambapo tunaona kila kitu
katika ulimwengu huu, sasa tunaweza kuona ulimwengu wa kiroho kwa wazi hasa
baada ya macho yetu ya kiroho kufunguliwa kwa kupitia imani yetu katika injili
ya maji na Roho. Hivi ndivyo mtu anavyoweza kuufikia ufahamu kwamba huduma ya Yesu
inahusu hasa huduma ya injili ya maji na Roho.
Kwa sababu ya dhambi zetu, wewe na mimi tulikuwa ni
vipofu na viwete wa kiroho, na kwamba hatukuweza kuiona huduma ya Mungu wala
kuifanya kazi yake. Kwa maneno mengine, sisi pia tulikuwa ni wenye dhambi ambao
tulikuwa tumefungwa ili kwenda kuzimu. Hata hivyo, Yesu Kristo alikja hapa duniani,
alibatizwa na Yohana Mbatizaji, akaimwaga damu yake Msalabani, na kwa sababu
hiyo akazitimiza kazi ambazo ziliondolea mbali dhambi zote za ulimwengu. Kwa
hiyo, yeyote atakayeamini katika Ukweli huu ataona bayana kuwa dhambi zake zote
zimeoshelewa mbali kikamilifu. Kwa kweli Yesu Kristo amezisafishilia mbali
dhambi zetu zote kwa kuja hapa duniani, kwa kubatizwa na Yohana Mbatizaji, na
kwa kuimwaga damu yake Msalabani.
Hata sasa, kazi hizo za Mungu, zinaendelea kujifunua
vizuri katika mioyo ya wale wote wanaoamini katika injili ya maji na Roho.
Bwana wetu ameyafunua macho ya waamini wake kiroho, na ametufanya sisi tuliokuwa
viwete kiroho, kuinuka na kusimama kwa miguu yetu kwa kupitia nguvu ya injili
ya maji na Roho.
Hapa tunahitaji kutambua kuwa ikiwa tutajaribu kuifanya
kazi ya Mungu pasipo kuwa na imani katika injili ya maji na Roho, basi ni hakika kuwa hakutakuwa na faida
yoyote kwa miili yetu wala kwa roho zetu. Wale ambao bado hawajapokea ondoleo
la dhambi zao wanafikiri wakati wote, “Ninapaswa kuishi maisha mema. Ninapaswa
kuwa mwema kwa kila mtu.” Lakini hakuna hata mmoja ambaye anaweza kulifanya
hili, yaani kutenda mema na kuishi maisha mema.
Kabla hatujaifahamu injili ya maji na Roho, tulikuwa
na dhambi katika mioyo yetu na kwa sababu hiyo sisi sote tulikuwa na dhambi
katika mioyo yetu na kwa sababu hiyo tulikuwa ni wenye dhambi, na hivyo
hatukuweza kuifahamu kazi ya Mungu ya haki ilivyo na wala hatukuweza kuitenda. Hata
hivyo, kwa kuwa Bwana wetu alizipokea dhambi zetu zote mara moja na kwa wote
kwa kupitia ubatizo wake, na kwa sababu alizisafishilia mbali kwa damu yake
aliyoimwaga Msalabani hali akiwa amejitwika dhambi za ulimwengu, basi hapo tuliweza
kuokolewa toka katika dhambi zetu zote.
Sasa tunaweza kuishi kwa mujibu wa mapenzi ya Mungu
kwa sababu Yesu Kristo ametuokoa toka katika dhambi kwa nguvu ya injili ya maji
na Roho. Sasa tunaweza kumwezesha yeyote yule kuionja radha ya nguvu ya
injili hii ya kweli na kisha kuokolewa.
Yesu Kristo ametuwezesha kuokolewa toka katika
dhambi na laana zetu zote kwa kuleta maisha mapya kwako wewe na mimi ambao
tulikuwa ni viwete kwa kupitia Ukweli wa wokovu. Alichosema Yesu hapa ni kuwa,
“wenye ukoma wanatakaswa na viziwi wanasikia; wafu wanafufuliwa,” kimetimizwa katika
mioyo yetu yote inayoamini katika injili ya maji na Roho.
Tulipokuwa tungali wenye dhambi, pia tulikuwa ni
wakoma wa kiroho. Wakati huo mioyo yetu ilikuwa na dhambi, na hatukuweza kusafishwa
toka katika dhambi zetu zote hadi pale tulipoiweka imani yetu katika injili ya
kweli ya maji na Roho.
Pia Bwana wetu alisema kuwa viziwi watasikia. Tulipokuwa
wenye dhambi, hatukuweza kulifahamu Neno la Mungu hata pale tuliposikia. Lakini
sasa, kwa kuwa tumefunikwa na nguvu ya injili ya maji na Roho kwa kuiweka imani
yetu juu yake, tunaweza kulifahamu Neno la Mungu, na kufahamu maana yake ya
kweli, na kisha kuliamini hilo Neno kwa mioyo yetu yote.
Kila mtu ulimwenguni pote anaishi katika njaa na kiu
ya kiroho. Watu wanateseka kutokana na upofu wa ulemavu wa kiroho. Lakini Bwana
bado anawapatia nafasi ya kuponywa mara moja kwa kuturuhusu kuwahubiria injili
ya maji na Roho. Ni lazima tuwaonee huruma. Tunahitaji kukumbuka kuwa wakati
tulipokuwa hatuifahamu injili hii ya wokovu, ambayo ni injili ya maji na Roho,
hatukuwa na ukamilifu, na kwamba hatukuweza kufanya lolote zaidi ya kuishi hali
tukiwa na dhambi zetu zote katika mioyo yetu. Hatupaswi kuisahau neema yake
yenye huruma ambayo imewageuza wenye dhambi kuwa wenye haki.
Kwa hiyo, kile ambacho Bwana wetu alikizungumza kwa
wanafunzi wa Yohana Mbatizaji kuhusu maajabu ambayo alikuwa anayatenda alikuwa na
lengo kuwafanya wafahamu kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mwokozi wa kweli na
Masihi atakayekuja. Baadhi wanaweza kusema kuwa wakati Yohana Mbatizaji
alipofungwa, alijaribiwa hadi akawa na mashaka ikiwa Yesu alikuwa ni Masihi
atakayekuja, na kwamba hii ndio sababu aliwatuma wanafunzi wake kwenda kwa
Yesu. Lakini hii si kweli.
Yohana Mbatizaji alikuwa ni nani? Alikuwa ni mkuu
kati ya wote waliozaliwa na wanawake. Alikuwa ni mkuu kuliko mtumishi mwingine
yeyote wa Mungu. Kwa maneno mengine, sio kwamba Yohana alikuwa hamwamini Yesu
kiasi kuwa akatuma wanafunzi wake kwenda kumuuliza, “Wewe ndiye yule ajaye?” Bali
alichokuwa anakifanya ni kuwaelimisha wanafunzi wake ili waweze kufahamu hasa
kuwa Yesu ni nani.
Yohana Mbatizaji alikwishaamini na kufahamu kuwa
Yesu ni Mwokozi na Mwana wa Mungu; zaidi ya yote, alikuwa amekwishasikia
ushuhuda wa Mungu Baba wakati alipombatiza Yesu Kristo katika Mto Yordani (Mathayo 3:17), na pia yeye mwenyewe alikuwa ni
shahidi aliyekuwa akimshuhudia Yesu. Yohana Mbatizaji aliwatuma wanafunzi wake
kwa Yesu kwa kuwa wanafunzi wake walikuwa hawamfahamu Yesu kikamilifu, na
alitaka kuwafundisha kuwa Yesu Kristo ndiye Mwokozi atakayekuja.
Kwa kweli
baada ya Yohana Mbatizaji kufahamu kuwa Yesu Kristo alikuwa ni Masihi atakayekuja,
alijaribu kuiondoa huduma yake na kuwapeleka wanafunzi wake kwa Bwana. Ili kumfunua
Yesu kwa taifa la Isareli, Yoahan Mbatizaji
alisema kuwa, “Yeye[Yesu] hana budi kuzidi, bali mimi kupungua” (Yohana
3:30).Kwa mfano, Andrea, ndugu wa Simoni Petro, alikuwa ni mwanafunzi wa
Yohana, lakini alimfuta Bwana mara baada ya kumsikia Yohana akimshuhudia Yesu (Yohana
1:40).
Hata hivyo, ubishi unaotolewa juu ya Yohana Mbatizaji
unaeleza mambo mengi yasiyo na maana hata pale ambapo hawamfahamu Yohana
Mbatizaji vizuri, huku wakidai, “Yohana Mbatizaji alikuwa ameshindwa.
Aliangukia katika majaribu na akashindwa
kumwamini Yesu. Imani yake ilivurugika baada ya kufungwa.” Lakini ndugu zangu
waamini, hampaswi kuiwekea mashaka imani ya Yohana Mbatizaji.
Yohana Mbatizaji na Yesu walikuwa na majukumu yao
ambayo walipaswa kuyatimiza pamoja kwa majaliwa ya Mungu Baba. Na majukumu haya
yalikuwa ni kubatiza na kubatizwa, huduma ambazo zilikuwa na lengo la kuitimiza
haki ya Mungu. Hii ndio sababu Yesu na Yohana Mbatizaji kila mmoja aliishuhudia
huduma ya mwenzake.
Mathayo 11:7-9
inasema, “Na hao walipokwenda zao, Yesu alianza
kuwaambia makutano habari za Yohana, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini?
Unyasi ukitikiswa na upepo? Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa
mavazi mororo? Tazama, watu wavaao mavazi mororo wamo katika nyumba za wafalme.
Lakini kwa nini mlitoka? Ni kuona nabii? Naam, nawaambia, na aliye mkuu zaidi
ya nabii.”Hapa Yesu alisema, “Kwa nini mlikwenda nyikani? Kumwona nabii?
Ikiwa ni hivyo, mpo sahihi. Ninawaambia kuwa Yohana Mbatizaji ni mba mkuu zaidi
ya nabii.” Kisha Yesu alimwelezea
Yohana Mbatizaji kwa kunukuu Malaki 3:1 katika Maandiko. Mathayo
11:10 ni kifungu kinachonukuu Malaki 3:1.
Katika kifungu hiki, Yesu alisema, “Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, mimi
natuma mjumbe wangu mbele ya uso wako, atakayeingeneza njia yako mbele
yako.”Kwa maneno mengine, kwa kunukuu kifungu kilichoandikwa katika Malaki 3:1, Yesu alishuhudia kuwa Yohana Mbatizaji alikuwa ni mtumishi halisi wa Mungu
ambaye ndiye aliyetumwa kumtangulia Yesu Mwenyewe. Mtumishi wa Mungu
aliyeandikwa katika Malaki 3:1 ni nani? Si
mwingine bali ni Yohana Mbatizaji. Malaki 4:5-6
pia inaonyesha kuwa mtumishi anayetajwa katika Malaki
3:1—“Namtuma
mjumbe wangu”—ina maanisha ni Yohana Mbatizaji. Katika Mathayo 11:11, Yesu alisema, “Amin, nawaambieni,
hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji; walakini
aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye.”
Kwa nini Bwana alituambia hili? Kwa nini alisema
kuwa Yohana Mbatizaji alikuwa ni mkuu kuliko wote waliozaliwa na wanawake? Hapa
Yesu anatueleza kuwa Yohana Mbatizaji
alikuwa ni mtumishi halisi wa Mungu aliyekuwa ametabiriwa katika Agano la Kale,
na kwamba yeye ni mwakilishi wa wanadamu. Kifungu hiki kinaendelea kwa kueleza
sentensi ngumu: “Walakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko
yeye.” Waalimu wengi wa uongo wanamhukumu Yohana Mbatizaji kuwa mtu aliyeshindwa
kwa kuangalia kifungu hiki. Wanadai “Kwa sababu Yohana alikuwa na mashaka kuhusu Yesu’
kuwa ni Masihi, na kwa sababu hiyo alitathminiwa na Bwana kuwa ni mtu wa
mwisho.” Madai haya ni upuuzi mtupu. Ila, kile anachokisema hapa Yesu ni
kwamba ingawa Yohana Mbatizaji alikuwa ni mwakilishi wa wanadamu, kwa upande wa
kiroho, alikuwa ni mtu wa chini ambaye hakuweza kufananishwa na wale waliokuwa
wamefanyika watoto wa Mungu. Kwa maneno mengine, pamoja na kuwa Yohana
Mbatizaji alikuwa ni mwakilishi wa wanadamu wote katika mwili, basi yeye hakuweza
kufananishwa na walele waliozaliwa tena upya.
Kwa kweli Yohana alikuwa ni mkuu katika mtazamo wa
kibinadamu. Yeye alilelewa kama Mnadhiri, na aliishi maisha ya kitawa akiwa
nyikani akila nzige na asali ya mwitu. Kutokana na mtazamo wa haki wa kibinadamu,
ni kweli kuwa Yohana alikuwa ni mkuu. Lakini hii haki ya kibinadamu haina maana
yoyote hasa pale inapolinganishwa na haki ya Mungu ambayo inaweza kutolewa kwa yeyote
anayeweza kuingia Ufalme wa Mungu kwa imani. Kwa sababu ya wale waliofanyika
kuwa watu wa Ufalme wa Mbinguni kwa kuamini katika injili ya maji na Roho
wameipokea haki ya Mungu, basi hao ni wakuu kuliko mtu yeyote anayeitegemea
haki yake binafsi. Mtu anaweza kuwa mwakilishi wa wanadamu katika ulimwengu huu
katika mwili, lakini yeye ni mdogo kuliko wale waliofanyika watu wa Mungu kwa
kuamini katika injili ya maji na Roho.
Hivyo basi, wakati Yesu aliposema, “Tangu siku za
Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni wapatikana kwa nguvu, na wenye
nguvu wauteka,”alisema hiyo kwa sababu Yohana Mbatizaji alikuwa
amembatiza mara moja na hivyo kuzipitisha dhambi za ulimwengu kwenda kwa Yesu. Kwa
hiyo, Yohanan Mbatizaji alikuwa ni Kuhani Mkuu wa wisho na nabii wa mwisho wa
Agano la kale, na huduma yake iliisha pale alipombatiza Yesu na akamshuhudia.
Kwa maneno mengine, Yesu anatueleza kuwa kila kitu cha Agano la Kale kiliisha kwa
kuonekana kwake na kwa kuonekana kwa Yohana Mbatizaji, na kwa huduma ya Yohana Mbatizaji
ya kumbatiza Yesu. Kwa lugha nyingine, tangu wakati ambapo Yohana Mbatizaji na
Yesu walikuja hapa ulimwenguni, hapo ndipo haki yote ya Mungu ilitimizwa.
Kipindi cha Agano Jipya kilifunguliwa wakati Yesu alipokuja hapa duniani na
kubatizwa na Yohana Mbatizaji.
Kipindi hiki
cha Agano Jipya ni kipindi cha nguvu ya injili, ni wakati ambapo yeyote anayeamini
katika injili ya maji na Roho anaweza kupokea ondoleo la dhambi na kufanyika
mwana wa Mungu. Kadri Agano la Kale lilivyodumu hadi siku za Yohana Mbatizaji,
wakati Yesu alipokuja hapa duniani, wakati alipozichukua dhambi za mwanadamu
kwa ubatizo wake, akaimwaga damu yake, na kuzitoweshea mbali dhambi zetu zote,
basi tangu hapo malango ya Mbinguni yamefunguliwa kwa wote wanaoamini katika
Ukweli huu.
Wakati Yesu alipozichukua dhambi zote za kila mmoja
katika ulimwengu huu kwa kubatizwa, basi hapo ndipo kipindi cha Agano Jipya
kilipoanza. Neno lote la unabii la Agano la Kale lilitimizwa kwa kupitia Yohana
Mbatizaji na kwa kupitia Yesu Kristo.
Yesu Kristo alizipokea dhambi zote za wanadamu mara
moja na kwa wote kwa kubatizwa na Yohana Mbatizaji, kisha akaimwaga damu yake
Msalabani, na kwa sababu hiyo amezitoweshea mbali dhambi zote za ulimwengu. Hii
ndio sababu Bwana wetu alisema tangu siku za YohanaMbatizaji hata sasa Ufalme
wa Mbinguni wapatikana kwa nguvu.
Yeyote anayeamini katika Ukweli huu anaweza kuingia
Mbinguni kwa imani kwa kuwa Yesu alizipokea dhambi za ulimwengu kwa kuupokea ubatizo
toka kwa Yohana Mbatizaji. Kwa lugha tofauti, Yesu aliweza kuzichukua dhambi
zote za wanadamu mara moja na kwa wote kwa kuwa Yohana Mbatizaji alikuwa
amezipitisha dhambi zote za mwanadamu kwenda kwa Yesu. Yohana Mbatizaji aliweza
kulitimiza jukumu la kuzipitisha dhambi za ulimwengu kwenda kwa Yesu akiwa kama
Kuhani Mkuu wa mwisho wa Agano laKale na hii ni kwa sababu Yohana Mbatizaji
alikuwa amezaliwa toka katika ukoo wa Haruni Kuhani Mkuu.
Kule kusema kila mtu anayeamini katika Ukweli huu
anaweza kuingia Mbinguni kwa imani ni kutokana na ukweli kuwa Yohana Mbatizaji
alikuwa amezipitisha dhambi zote za ulimwengu kwenda kwa Yesu kwa kumbatiza, na
pia ni kwa sababu Yesu alizichukua dhambi za ulimwengu na ndio maana kipindi
cha wokovu kwa mwanadamu kimetufikia. Kwa tukio hili la kihistoria, kipindi cha
Agano la Kale kiliisha, na kipindi cha Agano Jipya kilianza.
Yesu aliitimiza huduma yake kama Mwokozi wetu mkamilifu
kwa kuzichukua dhambi zetu zote za mwanadamu kwa ubatizo wake, na kwa kuimwaga damu
yake, na kwa kufufuka tena toka kwa wafu. Hivyo basi, wakati mpya umefika kwa
wale wote wanaoamini katika ubatizo ambao Yohana Mbatizaji aliutoa kwa Yesu,
ambapo Ufalme wa Mbinguni unapatikana kwa nguvu.
Ukweli ni kuwa Ufalme wa Mbinguni hauwezi kuchukuliwa
kwa nguvu ya kimwili. Sasa, maana ya kiroho ya kifungu hiki ni ipi? Maana yake
ni hii: Yesu anatueleza juu ya fumbo la Mbinguni, kwamba mtu yeyote anaweza
kuingia Mbinguni kwa kuamini katika injili hii kwa sababu Yesu alizipokea
dhambi zote za ulimwengu wakati Yohana Mbatizaji alipombatiza Yeye, na kwa
sababu ya kusulubiwa na kuimwaga damu yake na kufufuka tena toka kwa wafu.
Bwana wetu alisema, “Manabii wote na torati walitabiri hadi
wakati wa Yohana.”Kwa maneno mengine, unabii wa Agano la Kale ulidumu
hadi wakati wa Yohana Mbatizaji. Na kwa kweli ni sahihi kusema kipindi cha
Agano la Kale kilidumu hadi kuzaliwa kwa Yesu. Lakini unabii wa Agano la Kale
ulitimizwa kiroho wakati Yohana Mbatizaji alipombatiza Yesu.