Jumatatu, 10 Machi 2014

JENGA MADHABAHU KATIKA MOYO WAKO


Tunaweza kuona katika (kutoka 25:8-9) Nao wanifanyie patakatifu; ili nipate kukaa kati yao. Sawasawa na haya yote nikuonyeshayo, mfano wa maskani, na mfano wa vyombo vyake vyote, ndivyo mtakavyo vifanya.” (waebrania 3:6) “bali Kristo, kama mwana, juu ya nyumba ya Mungu; ambaye nyumba yake ni sisi, kama tukishikamana sana na ujasiri wetu na fahari ya taraja letu mpaka mwisho.”  kwamba Mungu alimwita Musa na akammwambia kupajenga mahali pa kuabudia ambapo Mungu ataishi. Mahali ambapo Mungu anaishi au kushinda hapo panaitwa madhabahu. Katika malango na katika mapaa ya madhabahu hii kulikuwa na fumbo lililokuwa limefichika, yaani fumbo la Yesu Kristo. Katika kifungu hiki ambacho Mungu aliwaamuru watu wa Israeli kuijenga madhabahu hii, basi ninaamini kuwa Mungu anatueleza sisi kuijenga madhabahu hii katika mioyo yetu ili kwamba aweze kuishi ndani yetu.
Nini ambacho tunapaswa kukifanya ikiwa tunahitaji Mungu akae ndani yetu? Kwanza kabisa, kwa kweli ni lazima tufahamu jinsi ambavyo Mungu alivyozisafisha dhambi zetu zote kwa kupitia Neno la Injili ya maji na Roho. Na ni lazima tuamini katika ukweli huo. Ili kufanya hivyo, kwanza ni lazima tuziangalie nafsi zetu kimsingi. Tangu kuzaliwa kwetu hatukuwa na chaguo jingine lolote bali kuzaliwa kama wenye dhambi. Inawezekanaje basi kwa Roho wa Mungu mtakatifu kukaa katika mioyo ya watu kama sisi? Ili Roho wa Mungu aweze kukaa katika mioyo ya wenye dhambi ni lazima  basi hawa wenye dhambi wawe na imani inayoamini katika Injili ya kweli. Kwa maneno mengine, Roho mtakatifu anakaa ndani yetu pale tu tunapokuwa tumezioshelea mbali dhambi zetu kwa kufahamu na kuamini katika Injili ya maji na Roho. Kule kusema kuwa Roho mtakatifu anaweza kukaa katika mioyo kumwezesha kwa kuamini katika ukweli wa milele wa maji na Roho.
Madhabahu ambapo Mungu anapenda kukaa
Hata hivyo, watu wengi ambao bado hawajapokea ondoleo la dhambi hawafahamu ukweli huu.  Unafikiri ni kwa nini Mungu alimwamuru Musa kulijenga Hema takatifu la kukutania? Alimwamuru Musa kwa sababu alitaka kukaa katika mioyo yetu. Tatizo ni kuwa watu wengi kutokana na kutojua kwao juu ya ukweli huu (Injili ya maji na Roho), wanatuimia kiasi kikubwa cha fedha kujenga majengo ya makanisa makubwa na ya kushangaza na wanadanganyika kuamini kuwa haya ndiyo mahekalu ambapo Mungu anaishi.
Watu wa jinsi hiyo wapo tayari kutoa fedha yote walioweza kuipata katika kipindi chote cha maisha yao kwa Mungu, kwa sababu wanafikiria kimakosa kuwa makanisa yao yanaweza kufanyika  ni mahekalu ya Mungu mtakatifu ikiwa kama watayajenga majengo ya kifahari na makubwa. Lakini je, ni kweli kuwa Mungu atapendezwa ikiwa tutajenga makanisa makubwa ya kupendeza na kisha tukampatia Mungu?. Je, ni kweli kuwa Mungu atakubaliki ikiwa utafanya jambo kama hili?  Je, kanisa hili litafanyika kuwa madhabahu ambayo inakaliwa na Mungu? Hivyo si kweli kabisa. Haya ni matokeo ya imani isiyofahamu ukweli wa Injili ya maji na Roho na walioangukia katika uongo mkuu.
Madhabahu ambayo Mungu anataka kuishi si jengo kubwa la kanisa bali ni moyo wako ambao umeoshwa dhambi zako. Mungu anapenda kukaa ndani ya mioyo ya wenye haki ambao wamepokea ondoleo la dhambi na waliofanyika watakatifu. Ili kulifanya hili liwezekane tunatakiwa kutoa sala zetu za toba ili tuweze kutakaswa? Hapana, kwa kweli siyo hivyo. Hata hivyo, kuna watu wengi wakristo wa siku hizi wanafikiri na kuamini namna hii.
Ili kulijenga Hema takatifu la kukutania kwa kupitia Musa, Mungu aliwaamuru wana wa Israeli kumtolea sadaka. Kama ilivyoandikwa katika (kutoka 25:3-7). Baada ya kuzipokea sadaka hizi kupitia Musa alijenga madhabahu ya Mungu kwa vifaa hivi kwa kupitia wafanyakazi ambao waliipokea hekima toka kwa Mungu. Kama ambavyo Mungu alimwamuru Musa kulijenga Hema takatifu la kukutania katika Agano la kale, basi katika Agano jipya, Mungu anatutaka sisi pia kujenga madhabahu katika mioyo yetu ili aweze kuishi ndani yetu. Vifaa vya imani ambavyo kwa hivyo tunaweza kuvitumia katika kuijenga madhabahu hii ni Neno la Injili ya maji na Roho. Kwa vifaa vya Injili hii ya maji na Roho ni lazima tuzioshelee mbali dhambi zetu zote na kusafishwa. Kwa kutueleza sisi kujenga madhabahu yake Mungu anatueleza sisi kuweka wazi moyo wako na kisha kuamini katika Injili ya maji na Roho.
Jambo hili sasa linazusha swali jingine juu ya aina ya imani ambayo tunapaswa kuwa nayo ili Mungu aweze kuishi katika mioyo ya wenye dhambi. Jibu ni rahisi na la wazi. Kwa kuwa Mungu mtakatifu aweze kuishi katika mioyo ya wenye dhambi, ni lazima kwanza wenye dhambi hawa wafahamu kile ambacho Injili ya maji na roho inawaeleza, na kisha ni lazima waamini katika ukweli huo. Ndipo mioyo yao inapoweza kusafishwa na kupokea ondoleo la dhambi, na ndipo hapo tu Mungu Mtakatifu anapoweza hatimaye kuishi katika mioyo ya watu wa jinsi hiyo ambao wamepokea ondoleo la dhambi wanapokuwa wameuachilia mbali ugumu wao na wakamini katika  Injili ya maji na roho, ambayo ni majaliwa ya Mungu, basi Mungu anaweza kuja na kukaa katika mioyo yao.
Hii ndiyo sababu 1wakorintho 3: 16-17 inasema, “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.” Mungu ni mtakatifu na asiye na dhmbi. Kwa hiyo, anaeza tu kuja katika mioyo yetu wakati inapokuwa imesafishwa vizuri kwa Neno la Injili ya maji na Roho. Biblia inasema kwa wazi kuwa ni wale tu waliopokea ondoleo la dhambi ndiyo wanaweza kupokea karama ya Roho Mtakatifu (Matendo ya mitume 2:38)
"Injili ya maji na Roho" inapatikana katika blog hii



Jumapili, 9 Machi 2014

BIRIKA LA KUNAWIA


(Kutoka 30:17-21) “BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Fanya na birika la shaba, na kitako chake cha shaba, ili kuogea; nawe utaliweka kati ya Hema takatifu la kukutania na madhabahu, nawe utalitia maji. Na Haruni na wanawe wataosha mikono yao na miguu yao humo; hapo waingipo ndani ya hema takatifu la kukutania; watajiosha majini, ili wasife; au hapo watakapoikaribia madhabahu ili watumike, kumtengenezea BWANA sadaka ya moto; basi wataosha mikono yao na miguu yao ili kwamba wasife; na neno hili litakuwa amri kwao milele, kwake yeye na kwa wazao wake katika vizazi vyao vyote.”
Birika la kunawia katika Ua wa Hema takatifu la kukutania
Vifaa: ilitengenezwa kwa shaba, ilikuwa imejazwa na maji wakati wote.
Maana ya kiroho: Shaba ina maanisha hukumu ya dhambi zote za mwanadamu, Yesu alizichukuwa dhambi za ulimwengu katika mwili wake kwa kubatizwa na Yohana. Kwa hiyo, maana ya birika la kunawia ni kwamba tunaweza kuoshwa dhambi zetu zote kwa kuamini kwamba dhambi hizi zote zilpitishwa kwa Yesu kwa kupitia ubatizo wake.
Makuhani waliohudumu katika Hema takatifu la kukutania pia waliosha mikono yao na miguu yao katika birika la kunawia kabla ya kuingia katika Hema Takatifu la kukutania na kwa hiyo walikiepuka kifo chao. Shaba inamaanisha hukumu ya dhambi, na maji ya kwenye birika la kunawia yanamaanisha ubatizo ambao Yesu aliopokea toka kwa Yohana na ambao kwa huo alizichuwa dhambi za ulimwengu katika mwili wake. Kwa maneno mengine, birika la kunawia linatueleza kuwa Yesu alizipokea dhambi zetu zote zilizopitishwa kwake na akabeba adhabu ya dhambi hizi. Maji katika birika la kunawia yanamaanisha, katika Agano la kale, nyuzi za bluu za hemataktifu la kukutania, na katika Agano jipya, ubatizo ambao Yesu aliopokea toka kwa Yohana (Mathayo 3:15, 1petro 3:21).
Kwa hiyo, birika la kunawia linamaanisha ubatizo wa Yesu, na ni mahali ambapo tunathibitisha imani yetu katika ukweli kuwa Yesu alibeba dhambi zetu zote, zikiwemo dhambi zetu halisi, na akazioshelea mbali zote mara moja kwa kupitia ubatizo alioupokea toka kwa Yohana Mbatizaji.
Watakatifu ambao wameokolewa toka katika dhambi zao kwa imani wamevishwa neema ya Mungu  kwa kuyaamini maji ya kwenye birika la kunawia (ubatizo wa Yesu), Shaba (hukumu ya Mungu kwa dhambi zote), na kwamba Yesu amewakomboa toka katika dhambi zao. Ingawa tuna wingi wa udhaifu na mapungufu kiasi kwamba hatuwezi kujitambua sisi wenyewe kuwa ni wenye haki, kwa hakika tunaweza kudhibitisha kwamba sisi ni wenye haki wakamilifu kwa kuiweka tena na tena imani yetu katika ubatizo wa Yesu (kuzibeba dhambi, maji) na damu yake iliyomwagwa msalabani (adhabu ya dhambi, shaba). Kwa sababu tunaliamini Neno la Mungu ambalo limekwisha kutuokoa sisi sote toka katika dhambi zetu na adhabu ya dhambi hizi, basi tunaweza kufanyika wenye haki wasio na dhambi.
Neno la Mungu tunaloliamini linatueleza sisi kuwa Yesu alizichukuwa dhambi zetu katika mwili wake kwa kupitia ubatizo wake alioupokea toka kwa Yohana, akamwaga damu yake msalabani ili kuibeba adhabu yote ya dhambi badala yetu, na kwa hiyo ametuokoa sisi kikamilifu toka katika dhambi zetu. Mungu aliliweka birika la kunawia katika ua wa Hema Takatifu la kukutania ili kwamba tuweze kudhibitisha kwa imani yetu kuwa sisi ndiyo tuliookolewa kikamilifu toka katika dhambi zetu zote bila kujali hali inavyoweza kuwa.
Matumizi ya birika la kunawia
Birika la kunawia lilitumika katika kuosha uchafu wote wa makuhani walipofanya kazi katika Hema Takatifu la kukutania wakitoa sadaka kwa Mungu. Ilihitajika kuyaosha madoa ambayo makuhani waliyapata katika kuua mwanasadaka wa kuteketezwa, katika kuikinga damu yake, na katika kuikata vipande ili kumtolea Mungu sadaka ambayo itawapatanisha watu wa Israeli na Mungu toka katika dhambi zao. Wakati makuhani walipochafuliwa walipokuwa wakitoa sadaka, iliwapasa kuoshwa kwa maji, na birika la kunawia lilikuwa ni mahali ambapo uchafu huu wote ulisafishwa.
Tunapofanya dhambi, kiroho au kimwili, na kila inapotokea kuwa tumechafuliwa kwa kuzivunja amri za Mungu, ni lazima tuoshelee mbali uchafu wetu wote katika birika hili la kunawia. Ilipotokea kuwa miili ya makuhani imegusa kitu chochote kichafu, walipaswa kwa lazima kuosha sehemu zilizochafuka katika miili yao kwa maji.
Vivyo hivyo, inapotokea kuwa wale wanaoamini katika Mungu wamegusana na kitu chochote kisicho safi na kichafu, maji ya birika la kunawia yanatumika kuoshelea mbali huo uchafu wote. Kwa kifupi, maji ya birika la kunawia yalitolewa ili yatumike katika kuuosha uchafu wa waliozaliwa upya. Kwa hiyo, birika la kunawia lina rehema za Mungu. Maana ya birika la kunawia si kitu cha kuchagua ambacho tunaweza kuchagua kuamini au kutoamini, bali ni kitu cha muhimu na lazima kwa wale wanaomwamini Yesu.
Mungu alitoa vipimo kwa vifaa vingine vyote katika Hema Takatifu la kukutania, akatoa vipimo maluumu jinsi ambavyo vitakuwa na dhiraa kadhaa kwa kimo, urefu, na upana. Lakini hakutoa kipimo cha birika la kunawia. Hii ni tabia ambayo inaapatikana tu katika birika la kunawia. Hii inadhihirisha upendo usiokoma ambao masihi ametupatia sisi, ambao tunatenda dhambi halisi kila siku. Katika upendo huu wa masihi  kunapatikana ubatizo wake, aina ya kuwekewa mikono ambayo inaziosha dhambi zetu zote. Kama ambavyo maji mengi yalitumika wakati makuhani walipokuwa wamechafuka wakati wakitekeleza majukumu yao, ilikuwa ni lazima birika la kunawia lijazwe maji wakati wote. Kwa hiyo, kipimo cha birika la kunawia kilitegemeana na hitaji hili. Kwa sababu birika la kunawia lilitengenezwa kwa shaba, basi kila ilipotokea makuhani wakinawa, walikuwa wanafikiria juu ya hukumu ya dhambi.
(Waebrania 10:22) inasema “tumeoshwa miili kwa maji safi”,  na (tito3:5) “ kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa mara ya pili na kufanywa upya na Roho mtakatifu.” Kama Vifungu hivi vinavyoonyesha, Neno la Agano Jipya pia linatueleza sisi kuhusu kuuosha uchafu kwa maji ya ubatizo.

Ikiwa makuhani waliosha uchafu wao walioupata katika maisha yao kwa maji ya birika la kunawia, sisi wakristo wa leo tuliozaliwa upya, tunaweza kuzioshelea mbali dhambi zetu Halisi zote zilizofanywa katika maisha yetu kwa kuamini ubatizo wa Yesu. Maji ya birika la kunawia la Agano la kale yanatuonyesha sisi kuwa Masihi alikuja hapa duniani na amezisafishaia mbali dhambi zote za ulimwengu kwa ubatizo aliopokea toka kwa Yohana.

Jumamosi, 8 Machi 2014

AGANO LA KALE Vs AGANO JIPYA


(2 Wakorintho 3:12-18), Basi kwa kuwa mna taraja la namna hii, twatumia ujasiri mwingi; nasi si kama Musa alivyotia utaji juu ya uso wake, ili kwamba Waisraeli wasitazame sana mwisho wa ile iliyokuwa ikibatilika; ila fikira zao zilitiwa uzito. Kwa maana hata leo hivi, wakati lisomwapo Agano la kale, utaji uo huo wakaa; yaani, haikufunuliwa kwamba huondolewa katika Kristo, ila hata leo, torati ya Musa isomwapo, utaji huikalia mioyo yao. Lakini wakati wowote watakapomgeukia Bwana, ule utaji huondolewa. Basi ‘Bwana’ ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru. Pia kifungu hiki kinapatikana (kutoka 34:34-36).
 Kwanini Musa alitia utaji juu ya uso wake? Ili Waisraeli wasitazame mwisho wa Agano la kale, ndiyo maana hata sasa mtu yeyote asomapo Agano la kale utaji uleule huukalia moyo wake. Lakini hata sasa ukiamini ya kuwa Agano la kale ni kivuli tu cha Agano jipya, basi utaokoka. Si kwamba Yesu alikuja kulitangua torati na manabii bali kulitimiliza (Mathayo 5:17). Kila jambo katika Agano la kale lina uhalisia wake katika Agano jipya “tafuteni katika kitabu cha BWANA mkasome hapana katika hao wote atakayekosa kuwapo, hapona mmoja atakayemkosa mwenzake; kwa maana kinywa changu kimeamuru na roho yake imekusanya” (Isaya 34:16). Tuangalie ni mambo gani watu wengi huyachanganya;
Mosi, nikweleze kwamba Biblia imeandikwa kwa uweza wa Roho mtakatifu, mtu yeyote asiye na Roho wa Bwana hata akeshe akisoma hawezi kuelewa (1wakorintho 2:10-15). Soma katika blog hii “Injili ya maji na roho” utaona ni jinsi gani unaweza kumpokea Roho mtakatifu. Wengi wamekuwa wakimwomba Mungu awape Roho mtakatifu kabla hawajaanza kusoma Biblia, lakini hilo halitakusaidia, maana Roho wa Bwana huja kwa imani iliyo sahihi tu. Mara unapoamini neno lililo sahihi utapokea Roho mtakatifu, wengine hudhani siku watakapo kwenda ndani ya maji ya ubatizo watapokea Roho mtakatifu lakini hilo si kweli maji ni ishara tu ya nje ya kile ulichokiamini ndani.
Pili, maswala ya sheria; hakuna mwanadamu yeyote awezaye kuishi kwa utimilifu kwa asilimia mia moja na kuitimiliza sheria, ukisoma Agano la kale (Walawi 4), utaona kwanini nasema hivi. Kumbe dhambi yeyote iwe ya kukusudia au ya kutokukusudia mbele ya Mungu ni dhambi. Ndiyo maana ukisoma (Warumi 7:14-16) “Kwa maana twajua ya kuwa torati asili yake ni ya rohoni; bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi. Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda. Lakini kama nikilitenda lile nisilolipenda, naikili ile sheria ya kuwa ni njema.
Hivyo mwili haufanyi jambo lolote jema. Mwili unatenda dhambi hadi unapokufa. Haijalishi jinsi unavyoweka umakini katika fikira zako na kujisemea moyoni, “sintafanya kitu kama hicho,” mwili hauwezi kukusaidia bali kutenda mambo maovu hata kinyume na vile unavyo penda. (Warumi 7: 25) “Kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi” katika Biblia kuna sheria za aina mbili; sheria ya Roho wa uzima na sheria ya dhambi na mauti (Warumi 8:2-3), sheria ya Roho wa uzima inapatikana katika haki ya Mungu itokanayo na ubatizo na damu ya Yesu. Wale wanaofikiri kuwa kumwamini Mungu ni kuishi kwa mujibu wa sheria hawawezi kuwa wakamilifu. “Kwa maana wale wafuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili”
Je, tutende dhambi kwa kuwa hatuko chini ya sheria ya dhambi na mauti? Hapana (Warumi 6:15), kwa kuwa utakuwa umeiamini haki ya Mungu, ile nguvu ya kuishinda dhambi itakuwa ndani yako, (waebrania 10:26-28) hivyo kutenda dhambi kwa kukusudia ni kosa kwako ambalo hautoweza kusamehewa. Si kwamba mwenye Roho wa Mungu hatendi dhambi, hapana, anatenda isipokuwa si kwa kukusudia (1Petro 3:21).
Katika Agano la kale Mungu aligawanya dhambi katika kukusudia na kutokukusudia, zile za kukusudia, hukumu yake ilikuwa ni kifo pasipo huruma na za kutokukusudia zilihitaji sadaka ya kuteketezwa ili kusamehewa. Hata sasa baada ya kuijua ile siri ya Mungu na Kumpokea Roho wa Mungu, ile nguvu ya kuishinda dhambi inakuwa ndani yako.
Ndiyo maana tunaokolewa bure kwa neema ya Mungu, Pale tunapozaliwa upya kwa ubatizo na damu ya Yesu. Wale wasioamini haki ya Mungu, lakini wako makanisani na wapagani hao wote neema ya Mungu haiwahusu, kwa maana hiyo watahukumiwa kwa sheria ya uzima na mauti.
Jambo la tatu:  imani bila matendo imekufa, kama tunaenenda kwa sheria ya “Roho wa uzima” na si kwa “sheria ya dhambi na mauti”  hivyo sheria ya matendo haitoweza kutuokoa kamwe, bali tunaokolewa kwa sheria ya imani, (Warumi 3: 21-28). Ukisoma waebrania 11 utaona tofauti iliyopo kati ya matendo ya imani na matendo ya sheria.
(Yakobo 2:21) “Je, Baba yetu Ibrahimu hakuhesabiwa kuwa na haki kwa matendo, hapo alipomtoa Isaka mwanae juu ya madhabahu? Waona kwamba ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na ya kwamba imani ile ilikamilishwa kwa njia ya matendo yale”.  Matendo yanayo ongelewa hapa si matendo ya sheria ni matendo ya imani.
Kwa hitimisho, kuna mifano mingi sana katika Biblia lakini kwa hiyo michache, unaweza kuwa umepata picha fulani ni nini Mungu anacho hitaji. Hivyo unapokea Roho mtakatifu kwa kuifahamu haki ya Mungu kwanza iliyo dhihirishwa katika ubatizo na damu ya Yesu, ndipo unapoweza kuenenda katika Roho.  (Wagalatia 5:22) “ lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”  unapokuwa umeshikamana na Roho wa Mungu mazingira katika ulimwengu wa Roho yanabadilika na kusababisha mazingira katika ulimwengu wa mwili pia kubadilika. Ndiyo maana hatuwezi kujisifia juu ya matendo yetu ya mwili mbele za Mungu.

Ungana nami katika masomo mengine kujifunza zaidi, katika agano la kale na jipya.






Ijumaa, 7 Machi 2014

MADHABAHU YA SADAKA YA KUTEKETEZWA.


(Kutoka 27: 1-8) “Nawe fanya madhabahu ya mshita; urefu wake utakuwa ni dhiraa tano; hivyo madhabahu itakuwa mraba; na kwenda juu kwake kutakuwa dhiraa tatu. Nawe fanya pembe nne; hizo pembe zitakuwa za kitu kimoja na madhabahu; nawe utayafunika shaba. Na vyombo vyake vya kuyaondoa majivu yake utavifanya, na majembe yake, na mabakuli yake, na uma zake, na meko yake; vyombo vyake vyote utavifanya vya shaba. Nawe uifanyie hiyo madhabahu wavu wa shaba; kisha utie pete nne za shaba katika hizo pembe nne za ule wavu. Nawe tia huo wavu chini ya kizigo kiizungukacho madhabahu upande wa chini, ili huo wavu ufikilie katikati ya hiyo madhabahu, miti ya mshita, na kuifunika shaba. Na hiyo miti itatiwa katika pete, na ile miti itakuwa katika pande mbili za madhabahu, wakati wa kuichukuwa. Uifanye ya mbao, yenye mvungu ndani yake; kama ilivyoonyeshwa mlimani, ndiyo watakavyoifanya.”
Tujadili juu ya imani inayodhihirishwa katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa. Wakati watu wa Israeli walipovunja mojawapo ya kanuni 613 za sheria ya Mungu na maagizo yake ambayo walipaswa kuyatii katika maisha yao ya kila siku, na walipozitambua dhambi zao walimtolea Mungu sadaka isiyo na mawaa kwa mujibu wa utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa  uliowekwa na Mungu. Mahali walipozitolea sadaka hizi ni katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa. Kwa maneno mengine, watu wa Israeli, walipokea ondoleo lao la dhambi kwa kuwekea mikono yao katika kichwa cha mnyama wa sadaka asiye na mawaa, na kwa kukata koo la mnyama na kuikinga damu yake, na kuiweka damu hiyo katika pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na kisha kuimimina ardhini damu iliyosalia, na hatimaye kumchoma mnyama huyo katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa.
Maana ya kiroho ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa .
Wakati Waisraeli walipoiangalia madhabahu hii ya sadaka ya kuteketezwa, ndipo walipotambua kuwa wao walikuwa wamefungwa katika kifungo cha hukumu (Shaba) na adhabu na kuwa wasingeweza kuikwepa hukumu yao. Na kama ambavyo mnyama wa sadaka ya kuteketezwa alivyouawa, ndipo walipotambua kuwa, hata wao walistahili kufa kwa sababu ya dhambi zao. Pia waliamini kuwa masihi atakuja hapa duniani na atazitowesha dhambi zao kwa kuwadhibiwa na kuuawa kama ilivyokuwa kwa mnyama wa sadaka ya kuteketezwa kwa sababu ya dhambi zao.
Madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa ilikuwa ni kivuli cha Yesu Kristo Mwokozi wetu. Kama ambavyo wanyama wasio na mawaa walivyouawa kwa kuwekewa mikono na kisha kumwaga damu yao, Yesu Kristo  alikuja kwetu kama Mwana wa Mungu na akabeba adhabu ya dhambi zetu zote. Kama ambavyo sadaka ya kuteketezwa ya Agano la kale alivyopokea dhambi zote kwa kuwekewa mikono na kumwaga damu, Yesu alizipokea dhambi zote za ulimwengu zilizopelekwa kwake  kwa kubatizwa na Yohana, na akabeba adhabu ya dhambi hizi kwa kuimwaga damu yake msalabani.
Kwa njia hii, madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa inatuonyesha sisi kuwa Yesu Kristo alizichukuwa dhambi zetu akafufuka toka kwa wafu, na kwa hiyo ametuokoa sisi.
Vyombo vyote vya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa vilitengenezwa kwa Shaba
Vyombo vya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa vilivyotumika kuweka na kuondoa majivu vyote vilitengenezwa kwa shaba. Madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa yenyewe ilitengenezwa kwa mti wa mshita na kisha ikafunikwa kwa shaba, na kwa hiyo madhabahu na vyombo vyake vyote vilitengenezwa kwa Shaba.
Shaba hii ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa ina maana kamili ya kiroho. Shaba inamaanisha hukumu ya dhambi mbele za Mungu. Kwa hiyo, madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa ni mahali panapotuonyesha vizuri kwamba wenye dhambi kwa hakika watahukumiwa kwa dhambi zao. Kwa hakika, Mungu atawaadhibu kwa dhambi zao pasipo kushindwa. Madhabahu hii ya sadaka ya kuteketezwa ni mahali ambapo wnyama wa sadaka ya kuteketezwa walihukumiwa kwa ajili ya wenye dhambi kwa kuteketezwa, madhabahu hii na Vyombo vyake vyote vilitengenezwa kwa shaba; kwa hiyo, vitu hivi vinatueleza sisi kuwa kwa hakika kila dhambi inahusisha hukumu yake.
Madhabahu inatuonyesha sisi kuwa kwa sababu ya dhambi zao, watu wamefungwa kuwadhibiwa na kisha kuuawa, lakini kwa kuwaleta wanyama wao wa kuteketezwa katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na kumpatia Mungu, wanaweza kuoshwa dhambi zao, kupokea ondoleo la dhambi, na kisha kuishi tena kwa upya.  Hapa, sadaka zilizoteketezwa katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa vyote vinatueleza kuwa ubatizo wa Yesu Kristo na kule kuimwaga damu yake kumezisamehe dhambi za waamini. Kwa hiyo, imani hii iliyotoa sadaka ya kuteketezwa katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa inaendelezwa katika kipindi cha Agano jipya kama imani katika ubatizo na damu ya Yesu Kristo.
Tunapomwamini Yesu Kristo kuwa ni mwokozi wetu, ni lazima tumpe Mungu imani Yetu inayoamini katika ubatizo na damu ya Yesu kama ondoleo la dhambi zetu zote. Katika Agano la kale, imani hii inahusianishwa na imani inayofungua na kuingia katika lango la ua wa Hema takatifu la kukutania lililokuwa limefumwa kwa nyuzi za bluu,zambarau, na nyekundu, na kitani safi ya kusokotwa.
Sadaka zote ambazo ziliteketezwa katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa ni kivuli cha Yesu Kristo.
Yesu Kristo alifanya nini alipokuja hapa duniani? Tulikuwa wenye dhmbi; tulikuwa tumetenda dhambi kinyume na Mungu na Tulikuwa tumevunja sheria na maagizo yake. Lakini ili kuzitowesha dhambi zetu, Yesu Kristo alibatizwa na Yohana na alichukuwa dhambi za ulimwengu katika mwili wake, na kwa hiyo akamwaga damu yake msalabani. Bwana wetu alibeba hukumu ya adhabu kwa dhambi zetu zote ili sisi tusiadhibiwe kwa dhambi zetu. Kwa hiyo, ametuokoa toka katika dhambi zetu zote na adhabu.
Pia kuna maana nyingine ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, ambayo ni “kupaa.” Kusema kweli, wewe na mimi tunatenda dhambi kila siku. Kwa hiyo, inatulazimu kutoa sadaka zetu za kuteketezwa kila wakati mbele za Mungu, na kwa sababu ya hali hii, moshi wa adhabu ya dhambi zetu kila siku unapaa kwenda kwa Mungu. Je, kuna siku yoyote ambayo hautendi dhambi bali unaishi kikamilifu? Sadaka ya kuteketezwa ya watu wa Israeli ilitolewa kila siku hadi pale makuhani walipochoka kuzitoa hizi ambazo zilileteleza msamaha wa dhambi za Waisraeli wengi. Kwa sababu watu wa Israeli walivunja sheria na wakafanya dhambi kinyume na Mungu kila siku, vivyo hivyo walipaswa kutoa sadaka zao za kuteketezwa kila siku.
Musa, akiwakilisha taifa la Israeli, alizitamka kanuni 613 za sheria na amri za mungu kwa Waisraeli; “sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika Agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kiliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu. Nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli” (kutoka 19:5-6).
Kisha watu wa Israeli wakaahidi, “hayo yote aliyoyasema BWANA tutayashika” (kutoka 19:8). Hivyo watu wa Israeli walitaka kumtambua na kumwamini huyu Mungu aliyemtokea Musa na akaongea nao kwa kupitia Musa kama Mungu wao Halisi, na walitaka Mungu huyu awalinde.  Kwa hiyo, walijitahidi kuzituza amri zote za Mungu ambazo aliwapatia.

Je, Mungu alifahamu mapema kuwa Waisraeli watatenda dhambi? Kwa kweli alifahamu. Hii ndiyo sababu Mungu alimwita Musa katika mlima Sinai, akamwonyesha Hema Takatifu la kukutania katika maono, akamweleza juu ya muundo wake wa kina, na kisha akamfanya Musa kulijenga kama alivyo mwamuru. Pia akaanzisha utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa ambao kwa huo sadaka zilipaswa kutolewa katika hili Hema Takatifu la kukutania.

Jumanne, 4 Machi 2014

HEMA TAKATIFU LA KUKUTANIA


Somo la tatu
Maana ya kiroho ya
Mti wa mshita, mafuta, na viungo
(Kutoka 25:1-9) “BWANA akanena na Musa, akamwambia: waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu. Sadaka utakayopokea mikononi mwao ni hii: dhahabu, na fedha, na shaba; na nyuzi za rangi ya bluu (samawiti), na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na kitani safi, na singa za mbuzi; na ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na ngozi za pompoo, na miti ya mshita; na mafuta ya ile taa, na viungo vya manukato kwa yale mafuta ya kupaka, na kwa ule uvumba wenye harufu nzuri; na vito vya shohamu, na vito vingine vya kutiwa kwa ile naivera, na kwa kile kifuko cha kifuani. Nao wanifanyie patakatifu; ili nipate kukaa kati yao. Sawasawa na haya yote nikuonyeshayo, mfano wa maskani, na mfano wa vyombo vyake vyote, ndivyo mtakavyo vifanya.”
Nguzo za hema takatifu la kukutania, madhahabu ya sadaka ya kuteketezwa, na mbao na vifaa vingine vya madhabahu vyote vilitengenezwa  kwa mbao za mti wa mshita. Kwa kawada mti katika Biblia unamaanisha wanadamu (waamuzi 9:8-15, marko 8:24). Pia mti hapa unamaanisha kwetu juu ya asili ya mwanadamu; ile hali ya kuwa mti huu wa mshita ulitumika katika nguzo, katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, na katika hema takatifu la kukutania lenyewe inatueleza kuwa kama ambavyo mizizi ya mti wa mshita mara zote imefunikwa ardhini, basi asili yetu ni ile ambayo haiwezi kujisaidi bali kutenda dhambi wakati wote. Ni lazima watu wote wakiri kuwa hawawezi kujisaidia bali wataendelea kuwa wasio na haki na kutenda dhambi kila mara.
Kwa wakati huo huo, mti wa mshita una maanisha juu ya ubinadamu wa Yesu Kristo. Masihi aliyekuja katika mwili wa binadamu alibeba dhambi zote za ulimwengu, na alihukumiwa kwa haki kwa ajili ya wanadamu. Yeye ni mungu mwenyewe, na kwa hiyo, sanduku la ushuhuda, meza ya wa wonyesho, madhabahu ya uvumba, na mbao za Hema takatifu la kukutania vyote vilitengenezwa kwa mti wa mshita na vikafunikizwa kwa dhahabu safi.
Mafuta kwa ajili ya mwanga na manukato kwa ajili ya mafuta ya kujipaka na kuwekea wakfu na kwa uvumba wa manukato vinamaanisha juu ya imani yetu ambayo tunaitoa kwa Yesu Kristo. Yesu Kristo ni masihi aliyetuokoa mimi na wewe. Maana ya jina “Yesu” ni “yeye atakaye waokoa watu wake toka katika dhambi zao,” na jina “Kristo” lina maana ya “mtiwa mafuta,” hivyo majina haya yanatueleza sisi kuwa Yesu Kristo ni Mungu mwenyewe na kuhahani mkuu wa Mbinguni aliyetuokoa sisi. Ili kuheshimu mapenzi ya Mungu, Bwana wetu alikuja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu, alibatizwa, alisulubiwa, msalabani  kwa ajili yetu, na kwa hiyo ametupatia zawadi ya wokovu. Kwa hakika jukumu la kuhani mkuu lililochukuliwa na Yesu aliye tupatia wokovu wetu lilikuwa ndiyo kazi nzuri sana.
Vito vya Shohamu, na Vito vingine vya kuwekwa katika Naivera na katika kile Kifuko cha kifuani cha kuhani mkuu.
Vito kumi na mbili vya aina tofauti vimetajwa hapa ambavyo vitawekwa katika naivera na katika kifuko cha kifuani cha kuhani mkuu. Kuhani mkuu alivaa kwanza gwanda kama kanzu fupi, kisha akavaa joho la bluu, na kisha akavaa naivera juu ya joho. Kisha, kifuko cha kifuani kiliwekwa katika naivera ambayo ilivaliwa wakati wa sherehe maalum ya sadaka ya kuteketezwa, na katika kifuko hiki cha kifuani viliwekwa vito kumi na mbili vya dhamani. Hii inatuonyesha sisi kuwa jukumu la kuhani mkuu lilikuwa ni kuwakumbatia na kuwa jumuisha wa Israeli pamoja na watu wengine wa ulimwengu mzima katika kifua chake, kwenda mbele za Mungu, na kumtolea mungu sadaka zao za kuteketezwa.
Yesu, ambaye ni kuhani mkuu wa milele wa Mbinguni pia aliyakumbatia mataifa yote ya ulimwengu katika kifua chake, akautoa mwili wake mwenyewe ili kuzichukuwa dhambi zetu kwa ubatizo wake na akasulubiwa kwa ajili yetu, na kwa hiyo amewaweka wakfu watu wake kwa Mungu Baba. Vito vya thamani kumi na mbili vilivyowekwa katika kifuko cha kifuani  vina maana ya mataifa yote ya ulimwengu huu, na kuhani mkuu aliye vaa vito hivyo ni alama ya Yesu Kristo ambaye amewaokoa mataifa na kuyakumbatia mataifa yote ya ulimwengu katika kifua chake.
Hivyo, hizi zilikuwa ni sadaka ambazo Mungu wetu aliwaambia Waisraeli kumtolea ili kulijenga hema takatifu la kukutania kwa jili yake. Kuna maana ya kiroho katika ukweli kuwa Mungu aliwaambia Waisraeli kumjengea hema takatifu la kukutania, mahali ambapo Mungu angeishi, kwa sadaka zao. Mara nyingi watu wa Israeli walibakia ni wenye dhambi kwa sababu hawakuweza kuitunza na kuifuata sheria ambayo Mungu aliwapatia. Hii ndiyo sababu Mungu aliwaeleza kupitia Musa kulijenga hema takatifu la kukutania  na kuwapatia utaratibu  wa sadaka ya kuteketezwa, ambayo kwa hiyo ondoleo la dhambi lilitolewa kwa sadaka ya kuteketezwa iliyotolewa katika Hema takatifu la kukutania. Kwa maneno mengine, Mungu alizifuta dhambi zote za Waisraeli kwa kuzipokea sadaka zao, kwa kutumia sadaka kuijenga nyumba yake, na kwa kuwafanya kumtolea sadaka zao za kuteketezwa katika Hema takatifu la kukutania kwa mujibu wa kanuni za utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa. Hivyo ndivyo ambavyo Mungu angeliweza kuishi katika Hema takatifu la kukutania pamoja na watu wa Israeli.
kumbuka tunapoongelea kulijenga hema takatifu, tunamaanisha vihi sasa wewe ni nyumba (hema) ya Mungu, vifaa vyote vilivyo agizwa na Mungu ni lazima hata sasa vitumike kukujenga kiroho kwa imani.
  


Jumatatu, 3 Machi 2014

MSINGI WA IMANI KATIKA UKRISTO


Somo la pili
Somo hili ni mwendelezo kutoka somo lenye kichwa “MSINGI WA IMANI ULIYOWEKWA NA VIFAA VYA UJENZI WA HEMA TAKATIFU LA KUKUTANIA”.
Sheria ni kivuli cha mambo mazuri yatakayo kuja, Vifaa vya ujenzi vya hema takatifu la kukutania vinatuonyesha sisi kuwa Bwana wetu alikuja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu, akazichukuwa dhambi zetu katika mwili wake, kwa ubatizo wake,akabeba adhabu ya dhambi zetu kwa kusulubiwa kwake, akafufuka tena toka kwa wafu, na kwa hiyo amefanyika kuwa mwokozi wetu.
 (Kutoka 25:1-9) “BWANA akanena na Musa, akamwambia: waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu. Sadaka utakayopokea mikononi mwao ni hii: dhahabu, na fedha, na shaba; na nyuzi za rangi ya bluu (samawiti), na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na kitani safi, na singa za mbuzi; na ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na ngozi za pompoo, na miti ya mshita; na mafuta ya ile taa, na viungo vya manukato kwa yale mafuta ya kupaka, na kwa ule uvumba wenye harufu nzuri; na vito vya shohamu, na vito vingine vya kutiwa kwa ile naivera, na kwa kile kifuko cha kifuani. Nao wanifanyie patakatifu; ili nipate kukaa kati yao. Sawasawa na haya yote nikuonyeshayo, mfano wa maskani, na mfano wa vyombo vyake vyote, ndivyo mtakavyo vifanya.”
MAANA YA KIROHO YA SINGA ZA MBUZI, NGOZI YA KONDOO DUME ILIYOTIWA RANGI NYEKUNDU, NA NGOZI YA POMPOO
Vifaa hivi vilitumika katika kujenga mapaa ya Hema takatifu la kukutania. Paa la kwanza lilifumwa kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa ambapo paa la pili la singa za mbuzi lililazwa. Kisha lilifunikwa kwa ngozi ya kondoo dume iliyotiwa rangi nyekundu na mwisho ngozi ya pompoo ililazwa juu yake. Kwa njia hii aina nne tofauti za tabaka la paa zililifunika hema takatifu la kukutania.
Paa la mwisho ambalo lilifunika Hema takatifu la kukutania lilikuwa la ngozi za pompoo. Kwa hiyo kilichoonekana katika uso wa paa la hema takatifu la kukutania lilikuwa ni hizi ngozi nyeusi za pompoo. Pompoo ni mnyama anayepatikana baharini. Kipimo cha ngozi ya pompoo ni kama kipimo cha mtu na pengine ni ndogo zaidi kuliko kipimo cha mtu, na aina hii ya ngozi ilikuwa haipitishi maji. Hii ndiyo sababu ngozi ya pompoo ilitumika kuezekea paa la Hema takatifu la kukutania. Kwa sababu ya hili, hali ya nje ya hema takatifu la kukutania Haikuwa ya kuvutia, na bila shaka halikuwa na mvuto wa kuangalia. Hii ianatueleza sisi kuwa wakati Yesu alipokuwa hapa duniani kwa ajili yetu, kwa hakika alikuja katika hali ya chini kama ilivyo kuwa hali ya nje ya hema takatifu la kukutania, hakukuwa na kitu cha kutamanisha katika mwonekano wake.
Ngozi ya kondoo dume iliyotiwa  rangi nyekundu inatueleza kuwa Yesu Kristo atakuja hapa duniani na atasulibiwa kwa ajili yetu, ilhali singa za mbuzi zinatueleza kuwa atatuokoa kwa kubatizwa kama sadaka yetu ya kuteketezwa na kwa hiyo atazipokea dhambi zetu katika mwili wake kwa kusulubiwa msalabani.
Lakini kwa sababu kuna watu wengi sana katika ulimwengu huu ambao imani yao haina ufahamu wowote kuhusu ubatizo wa Yesu, mara nyingi wamezidharau rangi nne za nyuzi zilizotumika katika hema takatifu la kukutania na badala yake wameyajenga malango yao ya hema takatifu la kukutania kwa nyuzi mbili tu.
Kwa kufanya hivyo wanawadanganya watu wengi, ambao tayari hawana uwelewa wa kutosha kuhusu Mungu na ambao hawajui kabisa neno lake. Hawa wote ni manabii wa uongo. Yesu mwenyewe aliwahi kuwazungumzia watu wa jinsi hii kwa kuwa ni magugu ambayo shetani aliyapanda katikati ya ngano (Mathayo 13:25). Kwa maneno mengine, wamekuwa ni watu ambao wanaeneza uongo kwa kuwacha nyuzi za bluu katika michoro yao ya ua wa Hema takatifu la kukutania. Hii ndiyo sababu watu wengi sana wanabakia ni wenye dhambi hata baada ya kuwa wanamwamini Yesu. Pamoja na imani yao katika Yesu bado wamefungwa katika uharibu kwa sababu ya dhambi zao.
Msingi wetu wa imani lazima uwe imara. Kuna uzuri gani kuishi kipindi kirefu cha maisha ya kidini katika nafsi yako ilhali maisha hayo yapo katika msingi usio wa sheria kiimani? Haijalishi kuwa nyumba zetu ni nzuri kiasi gani, kutakuwa na uzuri gani ikiwa tunajenga nyumba hizi katika msingi dhaifu wa kiimani? Bila kujali jinsi ambavyo umemtumikia Mungu kwa juhudi, ikiwa msingi wako wa imani una dosari, basi utakuwa umejenga nyumba yako katika mchanga; dhoruba itakapokuja na upepo kuvuma, na mafuriko yakaja, yataipiga nyumba yako nayo itaanguka chini mara moja.
Je, ni vipi kuhusu imani ya ambao msingi wao ni imara? Haitaanguka chini kamwe, hata ikitikiswa kiasi gani haitaanguka chini. Mungu alituambia sisi kuwa nyumba iliyojengwa katika mwamba wa kweli uliofumwa kwa nyuzi za bluu, zambarau, nyekundu na kitani safi ya kusokotwa haitaanguka chini kamwe. Na kwa kweli hivi ndivyo ilivyo. Je, imani ya mwamba ni nini? Ni imani inayo amini ukweli wa nyuzi za bluu, zambarau, nyekundu, na kitani safi ya kusokotwa. Imani ya watu waliojenga nyumba za jinsi hiyo za kiimani hazitaanguka kamwe. Na hii ndiyo sababu ni muhimu kwa imani yetu kuwa na msingi imara. Ikiwa hatuamini hata bila ya kufahamu vizuri yale ambayo Bwana amefanya kwa ajili yetu, basi imani ya jinsi hiyo itageuka kuwa imani ya kidini za uongo isiyotakiwa na Mungu.



Jumamosi, 1 Machi 2014

MSINGI WA IMANI ULIYOWEKWA NA VIFAA VYA UJENZI WA HEMA TAKATIFU LA KUKUTANIA

.
Somo la kwanza
(Kutoka 25:1-9) “BWANA akanena na Musa, akamwambia: waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu. Sadaka utakayopokea mikononi mwao ni hii: dhahabu, na fedha, na shaba; na nyuzi za rangi ya bluu (samawiti), na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na kitani safi, na singa za mbuzi; na ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na ngozi za pompoo, na miti ya mshita; na mafuta ya ile taa, na viungo vya manukato kwa yale mafuta ya kupaka, na kwa ule uvumba wenye harufu nzuri; na vito vya shohamu, na vito vingine vya kutiwa kwa ile naivera, na kwa kile kifuko cha kifuani. Nao wanifanyie patakatifu; ili nipate kukaa kati yao. Sawasawa na haya yote nikuonyeshayo, mfano wa maskani, na mfano wa vyombo vyake vyote, ndivyo mtakavyo vifanya.”
Baada ya Mungu kumpatia Musa amri kumi na sheria 613, kisha mungu akamwita Musa kwenda mlimani kwa mara nyingine, wakati huu alimwita ili kumwamuru kulijenga Hema takatifu la kukutania.
Kulikuwa na lengo mahususi ambalo kwa hilo Mungu alimwambia kuzileta sadaka hizi. Lengo hilo lilikuwa ni kuijenga hapa duniani nyumba ya Mungu yenye kung’aa, mahali ambapo hapana dhambi na ambapo Mungu atakaa , ili aweze kukutana na watu wa Israeli na kuzifanya dhambi zao kutoweka. Hata hivyo, hii haimaanishi kuwa Mungu aliwaeleza kuleta fedha ili kujenga jumba la kumbukumbu kama yalivyo makanisa ya leo. Manabii wa uongo wa Ukristo wa leo wanatumia kifungu hiki vibaya pale wanapotaka kuyajenga makanisa yao ili kuzitimiza tamaa zao binafsi.
Kwa kweli, sababu iliyomfanya Mungu apokee sadaka hizi ilikuwa ni kwa ajili ya kutukomboa sisi toka katika dhambi zetu na kutuokoa toka katika hukumu yetu. Pia ilikuwa kwa ajili ya Mungu ili aweze kukutana nasi, sisi ambao tulikuwa tukiishi maisha yenye huzuni ya kutisha, ili aweze kuziosha dhambi zetu na kuzifanya zitoweke, na kutufanya sisi kuwa watu wake mwenyewe.
MAANA YA KIROHO YA SADAKA AMBAZO MUNGU ALIAMURU ALETEWE
 Kabla hatujaenda mbali, hebu  tutumie muda kidogo kutafakari juu ya maana ya kiroho ya sadaka hizi ambazo Mungu aliamuru aletewe. Baada ya kutafakari tutaichunguza imani yetu kwa mtazamo wa sadaka hizo.
DHAHABU, FEDHA NA SHABA
Kwanza ni lazima tuchunguze mahali ambapo dhahabu, fedha, na shaba vilitumika. Katika Hema Takatifu la kukutania, dhahabu ilitumika kwa ajili ya mahali patakatifu, Patakatifu pa patakatifu, na vifaa vilivyokuwamo ndani ya hizo sehemu takatifu ikiwemo kinara cha taa, meza ya mkate wa wonyesho, madhabahu ya uvumba, kiti cha rehema, na snduku la ushuhuda.
Dhahabu inamaanisha neema ya wokovu. Inatueleza kuwa ni lazima  tuwe na imani inayoamini katika zawadi ya wokovu iliyotolewa bure na kwa ukamilifu na masihi, na imani ambayo inaamini kuwa Bwana wetu amezichukuwa dhambi zetu zote na kwamba alihukumiwa kwa ajili yetu.
Kwa upande mwingine, shaba, ilitumika katika vitanzi vya nguzo za Hema takatifu la kukutania, katika vigingi vyake, birika la kunawia, na madhahabu ya sadaka ya kuteketezwa. Vifaa au vyombo vyote vya shaba vilifunikwa au vilipigiliwa ardhini. Hii inamaanisha juu ya hukumu ya dhambi za watu, pia shaba inatueleza kuwa tunahukumiwa adhabu na Mungu kwa kushindwa kuitunza na kuifuata Sheria kwa sababu ya dhambi zetu.
Je, ni namna ipi ya kiroho ya dhahabu, fedha, na shaba? Vitu hivi vinaunda misingi ya imani katika kupokea zawadi ya wokovu iliyotolewa na Mungu. Biblia inatueleza kuwa sisi sote ni wenye dhambi ambao hatuwezi kuifuata sheria kikamilifu, na kwamba tunastahili kufa kwa sababu ya dhambi zetu kwa kufanyika sadaka ya kuteketezwa ya dhambi ambayo ilitolewa katika Hema takatifu la kukutania.
Ili kutatua tatizo la dhambi zao, wenye dhambi walileta mnyama asiye na mawaa katika Hema Takatifu la kukutania, na kwa mujibu wa taratibu wa sadaka ya kuteketezwa, walipeleka dhambi zao katika mnyama huyo wa sadaka kwa kuiwekea mikono yao juu ya kichwa chake; kisha sadaka ile ya kuteketezwa ambayo ilizipokea dhambi zao na kumwaga damu yake na kuuawa. Kwa kufanya hivyo, watu wa Israeli ambao walikuwa  wamefungwa kuzimu (shaba), waliweza kupokea ondoleo la dhambi zao (fedha), na walikwepa adhabu ya dhambi zao kwa imani (dhahabu).
NYUZI ZA BLUU (SAMAWITI), ZAMBARAU, NYEKUNDU NA KITANI SAFI YA KUSOKOTWA.
 Hapa kuna vifaa vingine vilivyotumika mara kwa mara; nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu, na kitani safi ya kusokotwa. Nyuzi hizi zilitumika katika lango la ua wa Hema takatifu la kukutania, lango la mahali patakatifu, na katika pazia lilotenganisha kati ya mahali patakatifu na patakatifu pa patakatifu. Nyuzi hizi nne zinatueleza juu ya ukweli kuwa kama ilivyo tabiriwa katika Mwanzo 3:15, kwamba Bwana atakuja kama sehemu ya uzao wa mwanamke, na kuwaokoa wenye dhambi toka katika dhambi zao kwa kubatizwa na kusulibiwa, na kwamba ni mungu mwenyewe ndiye atakaye tuokoa sisi.
Nyuzi nne hazikutumika tu kwa ajili ya malango ya Hema Takatifu la kukutania, bali zilitumika pia katika mavazi ya kuhani mkuu na yalitumika kama kifuniko cha kwanza cha Hema takatifu la kukutania. Hili lilikuwa ni Agano la mungu kwamba Yesu Kristo atakuja hapa duniani na kutuokoa toka katika dhambi zetu kwa kutimiza kazi zake za nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu. Kwa kweli Bwana wetu alitekeleza ahadi hii na kwa hakika ametuokoa toka katika dhambi za ulimwengu.
Sehemu ya msingi katika malango ya Hema takatifu la kukutania ni nyuzi za bluu. Kwanini Yesu Kristo kama masihi alikuja hapa duniani na kufa msalabani? Ni kwasababu Yesu alibatizwa. Nyuzi za bluu zinatuonyesha juu ya ubatizo wa Yesu, nyuzi za zambarau zinatueleza kuwa Yesu ni mfalme (Yohana 19:2-3),na nyuzi nyekundu zinatueleza juu ya kusulubiwa kwake na kumwaga damu yake. Nyuzi hizo zote ni vifaa vya ujenzi, ambavyo ni muhimu sana kutuonyesha jinsi Yesu alivyokuja hapa duniani na kuchua dhambi zetu katika mwili wake.
Watu wengi katika ulimwengu huu wanasisitiza kuwa Yesu ni mwana wa Mungu tu, na kwamba kimsingi yeye ni Mungu mwenyewe. Lakini anatueleza wazi kupitia Hema takatifu la kukutania kwamba mafundisho ya jinsi hiyo hayawezi kuwa ndiyo kweli kamili.
Mtume petro katika 1Petro 3:21, “mfano wa mambo hayo ni ubatizo, unao waokowa ninyi pia siku hizi; (siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamira safi mbele za Mungu), kwa kufufuka kwake Yesu Kristo.”
Hii inatuonyesha sisi kuwa Yesu aliitimiza ahadi ya wokovu na akaweka msingi wa imani mkamilifu kwa kupokea ubatizo wake, mfano unao tuokoa sisi. Masihi wetu ni nani? Maishi maana yake ni mwokozi, neno hili linatueleza kuwa Yesu alikuja hapa duniani, alibatizwa ili kuzichukuwa  dhambi zetu zote  na dhambi za ulimwengu katika mwili wake kwa njia ya  ubatizo.
Mungu aliwaeleza Waisraeli kulijenga lango la ua wa Hema takatifu la kukutania kwa kufuma nyuzi za bluu, zambarau na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Na dhumuni la Bwana wetu, ambaye ndiye mfalme wa wfalme na Bwana wa mbingu, kuja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu ilikuwa ni kuutimiza ukweli wa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Bwana wetu alikuja katika mwili wa mwanadamu na akaupokea ubatizo ambao ungeittimiza haki yote ya Mungu toka kwa Yohana Mbatizaji, ambaye ni mwakilishi wa wanadamu.
Hii inafanana na sadaka ya kuteketezwa ya Agano la kale ambayo ilizipokea dhambi za Waisraeli  ambazo zilipitishwa katika sadaka hiyo kwa kuwekewa mikono na kuhani mkuu katika kichwa chake na kwamba mnyama huyu wa sadaka alihukumiwa kwa dhambi hizo akiwa mbadala kwa dhambi za Waisraeli waliokosa. Kwa maneno mengine, kama ilivyo kuwa kwa sadaka ya kutetezwa ya Agano la kale, Yesu alikuja katika Agano jipya kama sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya dhambi za wanadamu, alibatizwa, alisulubiwa, na kwa hiyo alibeba adhabu yote ya dhambi za ulimwengu. Yesu aliutimiza ukweli wa nyuzi za bluu kwa kubatizwa na Yohana kama mwana kondoo wa Mungu wa sadaka. Kwa ubatizo huu Yesu alizichukuwa dhambi za wanadamu katika mwili wake mara moja na kwa wote.
Na nyuzi nyekundu zinamaanisha damu ya Yesu. Sababu iliyomfanya Yesu Kristo akasulubiwa, akamwaga damu yake, na akafa msalabani ni kwa sababu dhambi zetu zote zilikuwa zimepelekwa kwake kupitia ubatizo.  Ni kwa sababu Yesu alizichukuwa dhambi zetu kwa ubatizo wake alioupokea toka kwa Yohana Mbatizaji ndipo alipoweza kufa msalabani, na kwa sababu ya ukweli huu kwamba sadaka ya pale msalabani kwa ajili yetu haikuishia pasipo maana.
Nyuzi za zambarau zinamaanisha kuwa Yesu Kristo ni Mungu na mfalme, lakini kama asingebatizwa na Yohana Mbatizaji ambaye ni mwakilishi wa wanadamu, na kama asingelikuwa amezichukuwa dhambi zetu katika mwili wake (nyuzi za bluu), Haijalishi ni kwa kiwango gani cha mateso na maumivu aliyopata (nyuzi nyekundu), kifo chake kingekuwa hakina maana. Kitani safi ya kusokotwa inatueleza sisi kuwa neno la unabii ambalo Mungu aliliongea katika Agano la kale limetimizwa lote katika Agano jipya.

Soma mwendelezo wa somo hili………………