Alhamisi, 27 Machi 2014

UBATIZO KATIKA WOKOVU

                                        

 Tunapaswa kuzaliwa upya kupitia imani zetu, kukombolewa kutoka dhambini mwetu na kufanywa wenye haki. Na ndivyo pekee tunaweza kuingia katika ufalme wa milele Mbinguni Biblia inasema,“Amin, amin nakuambia, mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu” (Yohana 3:5) “Kuzaliwa upya kwa maji na Roho” ni njia pekee ya kuingia katika ufalme wa Mungu wa milele.
  Nini basi maana ya “kwa maji” na kwa “Roho” ambamo kunaruhusu kuzaliwa upya. “Maji” katika Biblia inamaanisha “ubatizo wa Yesu”
  Kwa nini Yesu aliye Mungu, alibatizwa na Yohana Mbatizaji? Je, ilikuwa ni kuonyesha unyenyekevu wake? Je, ilikuwa ni kutangaza kwamba yeye ni Masiha? La, hasha! Haikuwa hivyo.
  Wakati Yesu alipobatizwa na Yohana Mbatizaji kwa njia ya “kuwekewa mikono juu ya kichwa chake” (Walawi 16:21) ilikuwa ni “kitendo kiadilifu cha mtu mmoja” (Warumi 5:18) kinachotwalisha mbali dhambi za mwanadamu.
  Katika Agano la Kale, Mungu aliwapa Waisraeli sheria ya neema ya ukombozi. Hivi ndivyo ilivyo kuwa ile siku ya Upatanisho ambapo dhambi zote za Israeli katika mwaka huo zingelipiwa kwa maungamo kupitia Kuhani Mkuu Haruni, kwa kuwekea mikono yake kwenye kichwa cha mnyama wa kafara.
    Palikuwa na maneno ya ufunuo yaliyotabiriwa kuhusu sadaka ya ondoleo la dhambi milele. Ilionyesha ukweli kwamba dhambi za wanadamu zingetwaliwa kwa mara moja na Yesu aliye kuja katika mwili wa mwanadamu kutokana na mapenzi ya Mungu Baba. Na alibatizwa na Yohana Mbatizaji ambaye alikuwa ni wa uzawa wa Haruni na kuwa alikuwa mwakilishi wa wanadamu wote.
  Wakati Yesu alipotaka kubatizwa alimwambia Yohana “Kubali hivi sasa kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote” (Mathayo 3:15). Hapa neno“ndivyo itupasavyo” ina maana ya “kwa kuwekewa mikono”ni kwa nia ya kubebeshwa dhambi za ulimwengu kwa Yesu ili haki yote iweze kutimizwa kwetu sisi sote. Neno“haki” kwa Kigiriki “dikaiosune” lina maana ya “hali ya kustahiki”au “kuwa na stahili katika tabia au matendo katika kufanyizwa kuwa mwenye haki au kufaa”

Yesu alihimiza haki zote kwa niaba ya watu wote kwa kupitia ubatizo katika namna ya haki na stahili zote. Hivyo kwa kuchukua dhambi za watu wote kupitia ubatizo wake, siku iliyofuata baada ya ubatizo huo, Yohana Mbatizaji alishuhudia kwa kusema “Tazama Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!” (Yohana 1:29)
Kwa dhambi zote za wanadamu juu ya mabega yake, Yesu alitembea kuelekea msalabani. Kwa niaba alichukua hukumu ya dhambi alizo zibeba mwenyewe kupitia ubatizo wake. Alikufa msalabani hali akisema “Imekwisha” (Yohana 19:30). Kwake yeye mwenyewe alizibeba dhambi zetu sote na kupokea hukumu iliyo kamili kwa niaba yetu.
Maji, yakiwa na maana ya Ubatizo wa Yesu, ni Mfano wa mambo haya ya Wokovu.
  Hivyo, pasipo “kuwa na imani juu ya ubatizo wa Yesu” hatutookolewa. Na ndiyo maana Mtume Paulo alitamka kwamba “mfano wa mambo hayo ni ubatizo, unaowaokoa ninyi pia siku hizi” (1 Petro 3:21)
Siku hizi watu wengi wenye kumwamini Yesu hawauamini ubatizo wake wa “maji” bali huamini kifo chake tu, katika msalaba. Je, imani hii yaweza kweli kuokoa wenye dhambi? Je,itawezekana kweli kukombolewa kutoka kwenye dhambi zetu zote kwa kuamini Damu ya Yesu tu? Je, itaweza kutuletea wokovu wetu? Hasha! Hatutaweza kupata ukombozi wa Mungu kwa imani juu ya kifo cha Yesu msalabani pekee.
Wakati wana wa Israeli walipotoa sadaka ya upatanisho katika nyakati za Agano la Kale, isingekuwa njia sahihi kumchinja mnyama wa sadaka pasipo kwanza kuwekewa mikono juu ya kichwa chake kwa kutwikwa dhambi juu yake kwa niaba yao. Hivyo inakuwa ni kosa na kuvunja sheria ya Mungu kuamini msalaba wa Yesu pekee bila kuamini pia ubatizo wake.
Hivyo, Mtume Paulo alisema “Mfano wa mambo hayo ni ubatizo, unaowaokoa ninyi pia siku hizi; (siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamira safi mbele za Mungu), kwa kufufuka kwake Yesu Kristo. (1Petro 3:21) Kama ilivyo kwa wale walio acha kuamini “maji” makuu (mafuriko) nyakati za Nuhu waliangamizwa, ndivyo ilivyo kwa wale ambao hawata amini “maji” yaani “ubatizo wa Yesu” hakika wataangamia!
 Imani iliyo kamili ituongozayo kuelekea wakovu ulio wa kweli ni ile iliyo juu ya “aliyekuja kwa maji na damu, Yesu Kristo” (1Yohana 5:6) Yatubidi kuamini yote mawili, ubatizo na msalaba wa Yesu Kristo. Mtume Yohana alinena juu ya imani iliyo sahihi ni kuamini “ushuhuda wa Roho, maji na damu” (1Yohana 5:9)
  Kinachojenga na kubainisha imani iliyo ya kweli ni kuamini kwamba, “Yesu ni Mungu Halisi na alikuja katika mwili wa mwanadamu kwa uweza wa Roho kwa njia ya Mwanamwali Mariam na kubeba dhambi zetu zote kwa kubatizwa katika mto Yordan na Yohana Mbatizaji aliye kuhani mwakilishi wa wanadamu. Yesu alikwenda msalabani akiwa amezibeba dhambi zote za ulimwengu, na kupata hukumu isiyostahili kwake kwa ajili yetu” Hivyo basi, Injili haitoweza kukamilika pasipo “ubatizo wa Yesu” yaani “maji” Haijalishi ni kwa namna ipi iliyo sahihi una mwamini Yesu, pasipo kuamini jambo hili hautoweza kuingia katika wokovu wa milele. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni