Ijumaa, 14 Machi 2014

KUNA NJIA MOJA TU YA KUINGIA MBINGUNI


(Matendo 4:12) inasema, “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”
Kwa sababu tunaamini katika ubatizo wa Yesu na damu yake msalabani, basi sisi tutaingia Mbinguni. Hakuna njia nyingine ya kuingia Mbinguni bali kwa kuamini katika Injili ya kweli. Ni kwa kuamini tu katika yale ambayo Yesu amefanya kwa ajili yetu ndipo tunapoweza kuingia Mbinguni, kwa kuwa Mungu amefanya kazi hizo kwa wale wanaoamini katika Injili ya maji na roho (ipo katika blog hii).
Hii ndiyo sababu Wakristo hawawezi kuingia Mbinguni kwa kupitia jitihada zao wenyewe, kwa kujitoa, au majaribio mengine ya kinafiki. Mungu amedhamiria kuwa ni wale tu ambao wamesafishwa dhambi zao kwa kuamini katika ubatizo wa Yesu alioupokea na katika damu yake aliyoimwaga ndiyo wanaweza kuingia Mbinguni. Wale wanaoamini katika ukweli huu ndio wale wanaoamini kwamba Yesu ni mwana wa Mungu, Mungu mwenyewe, na mwokozi wa milele ambaye amewaokoa toka katika dhambi kwa kupitia ubatizo wake na damu yake aliyomwaga. Mungu ameruhusu kusafishwa dhambi kwa watu kama hao
Theolojia haina nafasi yoyote katika kuifahamu Biblia kiusahihi na kikamilifu. Theologja ni ufahamu wa kibinadamu si wa Roho mtakatifu. Ndiyo maana kuna lundo la mafundisho ya kikristo na theolojia  ambazo ziliinuka katika historia ya ukristo, watu wengi wameanguka katika mafundisho ya kimafumbo hali wakimwanini Mungu kwa kutegemea katika uzoefu wao binafsi. Lakini pamoja na tofauti za kitheolojia, matawi yote ya ukristo yametawaliwa na imani moja kimsingi, ambayo ni kuamini katika damu ya Yesu tu.
Lakini je, huu ni ukweli? Unapoamini kwa namna hii, je, dhambi zako zitatoweka kweli? Unafanya dhambi kila siku kwa moyo wako , mawazo, na matendo. Unaweza basi kuondolewa dhambi zako kwa kuamini katika damu ya Yesu tu ambayo alimwaga msalabani? Kule kusema kuwa Yesu alizibeba dhambi zetu kwa kubatizwa na kufa msalabani huo ni ukweli wa kibiblia. Hata hivyo kuna watu wengi sana ambao wanasema kuwa dhambi zao zimeondolewa kwa kuamini katika damu ya Yesu tu pale Msalabani na kwa kutoa sala zao za toba kila siku. Je, dhambi za dhamira zako zilisafishwa mbali kwa kutoa sala za toba za jinsi hiyo? Hii haiwezekani.
Ikiwa wewe ni mkristo, basi ni lazima ufahamu na kuamini katika wokovu wa kweli kwamba Yesu alikuja hapa duniani na akazichukuwa dhambi zetu zote za ulimwengu katika mwili wake kwa kubatizwa na Yohana. Pamoja na haya, je, bado unaudharau ukweli huu, kiasi kuwa hutaki hata kuufahamu na kisha kuamini? Ikiwa ndivyo, basi ufahamu kuwa unafanya dhambi ya kumdhihaki Yesu, dhambi ya kulishusha na kulidharau jina lake, na kwa jinsi hiyo huwezi kusema kuwa unaamini kweli katika Yesu kuwa ni mwokozi wako. Kwa kuuacha ubatizo wa Yesu Kristo na kwa kumwamini Yesu kwa namna yoyote unayoipenda, basi kwa kweli huwezi kuvikwa katika neema ya wokovu, (soma Injili ya maji na roho katika blog hii utaelewa nachokisema).
Njia ni moja tu ya kuingia Mbinguni (Mathayo 7:13-14) “ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache” kuna dini nyingi sana duniani ambazo zimefanikiwa kujikusanyia watu wengi kwa njia mbali mbali, usiangalie wingi wa watu, maana waionao njia ni wachache. Watu wengi wanapoteza muda kukosoa madhebu ya wengine, hata wale wasio wakristo mahubiri yao yamekuwa ni ya kukosoa ukristo.  Lakini ndugu unapoteza muda bure, Biblia si kama vitabu vingine ambavyo unaweza kuvisoma kwa kutumia akili za kibinadamu, inahitajika hekima ya Mungu, soma fungu hili (1wakorintho 2:10-15) lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu. Lakini sisi hatukupokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu. Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni. Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu”
Wale wanao ichambua Biblia kwa kutumia akili zao waache mara moja, wajisalimishe kwa Yesu, na wasome katika blog hii “Injili ya maji na roho” ili waweze kupokea Roho mtakatifu. Kuna wengine husoma na kudharau, lakini kumbuka bila Roho mtakatifu Biblia utaisoma kama kitabu cha hadithi na shetani atakufunga katika fikira zako. (2 Korintho 4:3-4) “lakini ikiwa Injili yetu imesitirka, imesitirika kwa hao wanaopotea, ambao ndani yao Mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao, isiwazukie nuru ya Injili ya utakatifu wake Kristo aliye sura yake Mungu”


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni