Jumamosi, 8 Machi 2014

AGANO LA KALE Vs AGANO JIPYA


(2 Wakorintho 3:12-18), Basi kwa kuwa mna taraja la namna hii, twatumia ujasiri mwingi; nasi si kama Musa alivyotia utaji juu ya uso wake, ili kwamba Waisraeli wasitazame sana mwisho wa ile iliyokuwa ikibatilika; ila fikira zao zilitiwa uzito. Kwa maana hata leo hivi, wakati lisomwapo Agano la kale, utaji uo huo wakaa; yaani, haikufunuliwa kwamba huondolewa katika Kristo, ila hata leo, torati ya Musa isomwapo, utaji huikalia mioyo yao. Lakini wakati wowote watakapomgeukia Bwana, ule utaji huondolewa. Basi ‘Bwana’ ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru. Pia kifungu hiki kinapatikana (kutoka 34:34-36).
 Kwanini Musa alitia utaji juu ya uso wake? Ili Waisraeli wasitazame mwisho wa Agano la kale, ndiyo maana hata sasa mtu yeyote asomapo Agano la kale utaji uleule huukalia moyo wake. Lakini hata sasa ukiamini ya kuwa Agano la kale ni kivuli tu cha Agano jipya, basi utaokoka. Si kwamba Yesu alikuja kulitangua torati na manabii bali kulitimiliza (Mathayo 5:17). Kila jambo katika Agano la kale lina uhalisia wake katika Agano jipya “tafuteni katika kitabu cha BWANA mkasome hapana katika hao wote atakayekosa kuwapo, hapona mmoja atakayemkosa mwenzake; kwa maana kinywa changu kimeamuru na roho yake imekusanya” (Isaya 34:16). Tuangalie ni mambo gani watu wengi huyachanganya;
Mosi, nikweleze kwamba Biblia imeandikwa kwa uweza wa Roho mtakatifu, mtu yeyote asiye na Roho wa Bwana hata akeshe akisoma hawezi kuelewa (1wakorintho 2:10-15). Soma katika blog hii “Injili ya maji na roho” utaona ni jinsi gani unaweza kumpokea Roho mtakatifu. Wengi wamekuwa wakimwomba Mungu awape Roho mtakatifu kabla hawajaanza kusoma Biblia, lakini hilo halitakusaidia, maana Roho wa Bwana huja kwa imani iliyo sahihi tu. Mara unapoamini neno lililo sahihi utapokea Roho mtakatifu, wengine hudhani siku watakapo kwenda ndani ya maji ya ubatizo watapokea Roho mtakatifu lakini hilo si kweli maji ni ishara tu ya nje ya kile ulichokiamini ndani.
Pili, maswala ya sheria; hakuna mwanadamu yeyote awezaye kuishi kwa utimilifu kwa asilimia mia moja na kuitimiliza sheria, ukisoma Agano la kale (Walawi 4), utaona kwanini nasema hivi. Kumbe dhambi yeyote iwe ya kukusudia au ya kutokukusudia mbele ya Mungu ni dhambi. Ndiyo maana ukisoma (Warumi 7:14-16) “Kwa maana twajua ya kuwa torati asili yake ni ya rohoni; bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi. Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda. Lakini kama nikilitenda lile nisilolipenda, naikili ile sheria ya kuwa ni njema.
Hivyo mwili haufanyi jambo lolote jema. Mwili unatenda dhambi hadi unapokufa. Haijalishi jinsi unavyoweka umakini katika fikira zako na kujisemea moyoni, “sintafanya kitu kama hicho,” mwili hauwezi kukusaidia bali kutenda mambo maovu hata kinyume na vile unavyo penda. (Warumi 7: 25) “Kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi” katika Biblia kuna sheria za aina mbili; sheria ya Roho wa uzima na sheria ya dhambi na mauti (Warumi 8:2-3), sheria ya Roho wa uzima inapatikana katika haki ya Mungu itokanayo na ubatizo na damu ya Yesu. Wale wanaofikiri kuwa kumwamini Mungu ni kuishi kwa mujibu wa sheria hawawezi kuwa wakamilifu. “Kwa maana wale wafuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili”
Je, tutende dhambi kwa kuwa hatuko chini ya sheria ya dhambi na mauti? Hapana (Warumi 6:15), kwa kuwa utakuwa umeiamini haki ya Mungu, ile nguvu ya kuishinda dhambi itakuwa ndani yako, (waebrania 10:26-28) hivyo kutenda dhambi kwa kukusudia ni kosa kwako ambalo hautoweza kusamehewa. Si kwamba mwenye Roho wa Mungu hatendi dhambi, hapana, anatenda isipokuwa si kwa kukusudia (1Petro 3:21).
Katika Agano la kale Mungu aligawanya dhambi katika kukusudia na kutokukusudia, zile za kukusudia, hukumu yake ilikuwa ni kifo pasipo huruma na za kutokukusudia zilihitaji sadaka ya kuteketezwa ili kusamehewa. Hata sasa baada ya kuijua ile siri ya Mungu na Kumpokea Roho wa Mungu, ile nguvu ya kuishinda dhambi inakuwa ndani yako.
Ndiyo maana tunaokolewa bure kwa neema ya Mungu, Pale tunapozaliwa upya kwa ubatizo na damu ya Yesu. Wale wasioamini haki ya Mungu, lakini wako makanisani na wapagani hao wote neema ya Mungu haiwahusu, kwa maana hiyo watahukumiwa kwa sheria ya uzima na mauti.
Jambo la tatu:  imani bila matendo imekufa, kama tunaenenda kwa sheria ya “Roho wa uzima” na si kwa “sheria ya dhambi na mauti”  hivyo sheria ya matendo haitoweza kutuokoa kamwe, bali tunaokolewa kwa sheria ya imani, (Warumi 3: 21-28). Ukisoma waebrania 11 utaona tofauti iliyopo kati ya matendo ya imani na matendo ya sheria.
(Yakobo 2:21) “Je, Baba yetu Ibrahimu hakuhesabiwa kuwa na haki kwa matendo, hapo alipomtoa Isaka mwanae juu ya madhabahu? Waona kwamba ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na ya kwamba imani ile ilikamilishwa kwa njia ya matendo yale”.  Matendo yanayo ongelewa hapa si matendo ya sheria ni matendo ya imani.
Kwa hitimisho, kuna mifano mingi sana katika Biblia lakini kwa hiyo michache, unaweza kuwa umepata picha fulani ni nini Mungu anacho hitaji. Hivyo unapokea Roho mtakatifu kwa kuifahamu haki ya Mungu kwanza iliyo dhihirishwa katika ubatizo na damu ya Yesu, ndipo unapoweza kuenenda katika Roho.  (Wagalatia 5:22) “ lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”  unapokuwa umeshikamana na Roho wa Mungu mazingira katika ulimwengu wa Roho yanabadilika na kusababisha mazingira katika ulimwengu wa mwili pia kubadilika. Ndiyo maana hatuwezi kujisifia juu ya matendo yetu ya mwili mbele za Mungu.

Ungana nami katika masomo mengine kujifunza zaidi, katika agano la kale na jipya.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni