Jumatano, 19 Machi 2014

FUMBO LA KIROHO KATIKA SANDUKU LA USHUHUDA


(Kutoka 25: 10-22) “Nao na wanifanyie sanduku la mti wa mshita; urefu wake na uwe dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu. Nawe ulifunike kwa dhahabu safi, ulifunike ndani na nje, nawe tia na ukingo wa dhahabu kulizunguka pande zote. Nawe subu vikuku vinne vya dhahabu kwa ajili yake, na kuvitia katika miguu yake minne; vikuku viwili upande mmoja, na vikuku viwili upande wake wa pili. Nawe fanya miti mirefu ya mshita na kuifunika dhahabu. Nawe tia hiyo miti katika vile vikuku vilivyo katika pande mbili za sanduku ili kulichukuwa hilo sanduku. Hiyo miti itakaa katika vile vikuku vya sanduku; haitaondolewa. Kisha tia ndani ya sanduku huo ushuhuda nitakaokupa. Nawe fanya kiti cha rehema cha dhahabu safi; urefu wake utakuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu. Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema. Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku. Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayo kuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli.”
Sanduku hili lilitengenezwa kwa mti wa mshita na lilifunikwa kwa dhahabu safi. Ndani ya sanduku kulikuwa na mbao mbili za mawe zilizokuwa zimeandikwa Amri kumi na birauli ya dhahabu iliyokuwa na mana, na baadaye iliwekwa ile fimbo ya Haruni iliyochipuka. Je, vitu hivi vitatu vilivyowekwa ndani ya sanduku hili la ushuhuda vinatueleza nini?
Mbao mbili za mawe zilizokuwa zimeandikwa sheria
Mbao mbili za mawe zilizokuwa zimeandikwa Sheria na kuwekwa ndani ya sanduku la ushuhuda zinatueleza sisi kuwa Mungu ndiye mtunga sheria ambaye ametupatia sisi sheria zake. (Warumi 8: 1-2) “ sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti.” Katika kifungu hiki tunaweza kuona kuwa Mungu alianzisha sheria mbili katika mioyo yetu: sheria ya uzima na sheria ya adhabu.
Kwa sheria hizi mbili, Bwana ameleta adhabu na wokovu kwa wanadamu wote. Kwanza kabisa tunaweza kutambua kwa kupitia sheria kwamba sisi tu wenye dhambi ambao bila kukwepa tumepangiwa kuzimu. Hata hivyo, kwa wale ambao wanaifahamu hali yao ya asili kuwa wamepangiwa mabaya, Mungu amewapatia watu wa jinsi hiyo sheria yake ya wokovu, “sheria ya Roho wa uzima katika Kristo Yesu” Mungu amefanyika kuwa mwokozi wa kweli kwa watu wote kwa kuwapatia sheria hizi mbili.
Maana ya kiroho ya bilauri ya dhahabu
Ile Bilauri ya dhahabu iliyokuwepo katika sanduku la ushuhuda ilikuwa na mana. Wakati watu wa Israeli walipotumia miaka 40 katika jangwa na nyika, Mungu aliwaletea chakula toka Mbinguni na Waisraeli waliishi kwa kutegemea mana hii wakiipika katika hali tofauti. Mana hii ilikuwa ni nyeupe kama vile mbegu za giligilani, na radha yake ilikuwa ni kama maandazi yaliyotengenezwa kwa asali. Hii mana ambayo Mungu alikuwa amewapatia watu wa Israeli iliwawezesha kuishi maisha yao hadi pale walipoingia katika nchi ya kanaani. Kwa hiyo, chakula hiki kiliwekwa kwa ajili ya ukumbusho na hivyo ikawekwa katika bilauri hii.
Hii inatueleza kuwa sisi waamini wa leo tunapaswa pia kula mkate wa uzima, ambao wana wa kiroho wa Mungu ni lazima waule wanapokuwa hapa duniani hadi pale watakapoingia Mbinguni. Lakini kuna nyakati ambapo tunapenda kuupata mkate wa ulimwengu, ambao ni mafundisho ya ulimwengu huu badala ya Neno la Mungu. Pamoja na hayo, kitu ambacho watoto wa Mungu wanapaswa kukiishia na kuishi kwa hicho hadi pale watakapofikia nchi ya kiroho ya kanaani  ni neno la Mungu, ambalo ni mkate wa kiroho wa maisha ya kweli unaotoka Mbinguni.
Mtu hawezi kuchoka kwa kuula mara kwa mara mkate wa maisha ya kweli. Kadri tunavyo upata mkate huu wa kiroho, ndivyo mkate huo unavyofanyika kuwa maisha ya kweli katika nafsi zetu. Lakini ikiwa tunaula mkate wa mafundisho ya ulimwengu badala ya Neno la Mungu, basi hatimaye nafsi zetu zitaishia mautini.
Mungu aliwaamuru watu wa Israeli kuiweka mana iliyotoka Mbinguni katika bilauri ya dhahabu na kuitunza. Kama inavyoonyeshwa katika kutoka 16:33, Mungu alisema, “ twaa kopo, ukatie pishi moja ya hiyo mana ndani yake uiweke mbele ya BWANA, ilindwe ka ajili ya vizazi vyenu.” Ile mana iliyotoka Mbinguni ulikuwa ni mkate wa maisha ya kweli kwa ajili ya nafsi za watu. “ Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali ishi kwa kila litokalo katika kinywa cha BWANA” (kumbukumbu la torati 8:3)
Mkate wa uzima kwetu sisi ni nani?
Ubatizo ambao Yesu Kristo aliopokea ili kuzichukua dhambi zetu katika mwili wake na kusulubiwa kwake na kuimwaga damu yake hivyo ndivyo vinavyo ufanya mkate wetu wa kweli wa maisha. Kwa kutupatia sisi mwili na damu yake, Yesu Kristo amefanyika kuwa ni mkate wa uzima wa milele. Kama ambavyo Yohana 6: 48-58 inatueleza sisi: “ Mimi ndimi chakula cha uzima. Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa,. Hiki ni chakula kishukacho kutoka Mbinguni, kwamba mtu akile wala asife. Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka Mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. ……………………………………………………………… endelea katika Biblia”
Mwili na damu ya Yesu katika Biblia, mwili wa Yesu unatueleza sisi kuwa Yesu Kristo alizichukuwa dhambi za ulimwengu katika mwili wake kwa kubatizwa na Yohana katika mto Yordani.  Na damu ya Yesu inatueleza sisi kuwa kwa sababu Yesu alibatizwa, basi alizuchukua dhambi za ulimwengu na akabeba adhabu ya dhambi za ulimwengu na akabeba adhabu ya dhambi hizo kwa kusulubiwa.
Mana katika ile bilauri iliyokuwa imewekwa ndani ya Sanduku la Ushuhuda ilikuwa ni mkate wa uzima kwa Waisraeli walipokuwa nyikani,na katika kipindi cha Agano Jipya, maana yake ya kiroho ina maanisha juu ya mwili wa Yesu Kristo. Ukweli huu unatuonyesha sisi ubatizo ambao kwa huo Yesu Kristo aliyachukuwa makosa na maovu ya wenye dhambi wote na damu ambayo aliimwaga pale msalabani. Kwa kuwa Yesu Kristo alichukuwa dhambi zote za ulimwengu huu katika mwili wake kwa kupitia ubatizo wake na damu yake iliyomwagika vimefanyika kuwa vitu muhimu vya kudumu vinavyowawezesha waaamini kuzaliwa tena upya.
Mwili ambao Yesu aliutoa ili kuyachukua maovu yote ya wenye dhambi kwa kupitia ubatizo wake na damu yake aliyoimwaga msalabani ni mkate wa uzima unaowawezesha wenye dhambi kupokea ondoleo la dhambi. Kwa hiyo ni lazima tutambue sababu ambayo ilimfanya Yesu kusema, “ msipoula mwili wake Mwana wa adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu” (Yohana 6:53).
Maelezo ya ziada; ni kwa kuamini katika ukweli huu halisi ndipo tunapoweza kuula mwili wake na damu yake. Kuoshwa kwa dhambi kulitimizwa pale ambapo dhambi za mwanadamu zilipopitishwa katika mwili wa Yesu kwa kupitia ubatizo ambao aliopokea. Kuinywa damu yake kunamaanisha kuwa Yesu alibatizwa na kuimwaga damu yake msalabani, damu hii aliyoimwaga ilibeba adhabu ya dhambi zetu.
Fimbo ya Haruni iliyochipuka
Miongoni mwa vitu vilivyowekwa ndani ya sanduku la ushuhuda, fimbo ya Haruni iliyochipuka ina maanisha juu ya Yesu Kristo kuwa ni kuhani mkuu wa milele wa ufalme wa mbinguni.  Pia inatueleza sisi kuwa uzima wa milele unaopatikana katika Yesu Kristo. Soma (Hesabu 16:1-2) Basi kora, mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatatwaa watu pamoja na dathani na abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi,waliokuwa wana wa Reubeni. Nao pamoja na watu kadha wa kadha wa wana wa Israeli, watu mia mbili na hamsini, Wakuu wa mkutano, waliokuwa wateule wa mkutano, watu wenye sifa, wakainuka mbele za Musa”.
Kifungu hiki kinatueleza sisi kuwa miongoni mwa Walawi, viongozi mashuhuri 250 wa watu walijikusanya na kuinuka dhidi ya Musa. Wakamwambia, “Musa na Haruni mmetufanyia nini kwa kutuongoza sisi toka katika nchi ya Misri? Je, mmetupatia mizabibu? Mmetufanyia nini? Je, hamkutuletea sisi huku nyikani ili hatimaye tufe katika jangwa la mchanga? Je, mwawezaje kujiita ninyi wenyewe kuwa ni watumishi wa Mungu? Je, Mungu anatenda kazi kwa kupitia ninyi tu?” kwa maneno mengine, kulikuwa kumeinuka upinzani na uasi dhidi ya uongozi wa Musa na haruni.
Kwa wakati huo, Mungu akamwambia Kora, Dathani, Oni, na viongozi wengine wa watu waliokuwa wameongoza uasi, “Niletee fimbo kutoka katika kila nyumba ya baba na andika kila jina la nyumba hiyo katika fimbo hiyo. Kisha ziweke hizo fimbo katika Hema takatifu la kukutania. Ziache pale kwa usiku mmoja na kisha uje kuziangalia siku inayofuata.” Kisha Mungu akasema, “Kisha itakuwa, mtu huyo nitakayemchagua, fimbo yake itachipuka; name nitayakomesha kwangu manung’uniko ya wana wa Israeli, wanung’unikayo juu yenu” (hesabu 17:5). Katika aya ya 8, tunaona kuwa “ilefimbo ya Haruni iliyokuwa kwa nyuma ya Lawi ilikuwa imechipuka, imetoa michipukizi, na kuchanua maua; na kuzaa milozi mabivu”.
Kisha katika aya ya 10, tunaona kuwa, “kisha BWANA akamwambia Musa, irudishe fimbo ya Haruni mbele ya ushahidi, ili ituzwe iwe ishara juu ya hawa wana wa maasi; ili uyakomeshe manung’uniko yao waliyoninung’unikia, ili wasife.”  Hivi ndivyo ambavyo fimbo ya Haruni iliyochipuka ilivyo kuja kuwekwa ndani ya sanduku la ushuhuda.
Hii inaonyesha kuwa Haruni wa ukoo wa Lawi alipakwa mafuta kuwa kuhani mkuu wa watu wa Israeli.musa alikuwa ni nabii wa Mungu na Lawi pamoja na ukoo wake wake walikuwa ni makuhani wakuu wa watu wa Israeli. Mungu mwenyewe alikuwa amewakabidhi majukumu ya kuhani mkuu wa kidunia Haruni. Mungu alikuwa amemwonyesha Musa utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa, ambapo watu wa Israeli walileta sadaka ya kuteketezwa na kumtolea Mungu kila walipofanya dhambi, na Mungu alimfanya Haruni kusimamia utoaji wa sadaka hizi kwa mujibu wa kanuni za utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni