Jumapili, 16 Februari 2014

SALA YA TOBA ITAWEZA KUTAKASA DHAMBI ZETU


Hakika sala ya toba haitoweza kamwe kutakasa dhambi zetu kwa sababu ukombozi hauwezi kuja kwa kupitia matendo yetu. Bali, ili tuweze kuwa wenye haki kamili na wakati wote tukiwa tumeoshwa dhambi zetu zote, yatupasa kuamini katika ubatizo na damu ya Yesu, na kuamini kuwa Yesu ni Mungu. Ukombozi kamili hupatikana kwa wale tu wenye kuamini kuwa Yesu alibeba dhambi zetu zote kwa ubatizo wake na kutoa damu yake msalabani kutupa uhai mpya.
Sasa basi, je tutaweza kutakasa dhambi zetu za kila siku kwa kufanya sala za toba kila mara? Hapana. Dhambi zote tuzitendazo maishani mwetu kila siku zilikwisha takaswa takribani miaka 2000 iliyopita pale Yesu alipozibeba kwa ubatizo wake. Hakika tumepata utakaso wa kudumu kwa dhambi zetu zote kwa ule ubatizo wa Yesu na kwa damu yake pale msalabani. Amekuwa mwanakondoo wa sadaka kwa ajili yetu wenye kumwamini, kusafishwa dhambi zetu zote, na kulipia yote kwa ubatizo na kwa damu yake msalabani.
Kwa lugha nyepesi, katika Agano la kale kuhani mkuu alikuwa akitoa sadaka ya upatanisho wa dhambi kila siku ya kumi ya mwezi wa saba (Walawi 16: 29-34). Aliye husika kumbebesha (kumtwika ) mnyama dhambi za Israel ni kuhani mkuu peke yake kwa niaba ya watu wote. Watu wa Israel hawakuwa na haja ya kila mmoja kuwekea mikono katika sadaka ya dhambi, bali walitakiwa kuamini kuwa dhambi zao zimesamehewa kupitia mwakilishi wao. Katika Agano jipya Yohana Mbatizaji amesimama (kama kuhani mkuu) badala ya watu wote ulimwenguni, hivyo alimtwika Yesu dhambi zetu zote katika ubatizo, nasi pia tunahitajika kuamini katika yale aliyofanya Yohana Mbatizaji (kuhani mkuu) na Yesu (mnyama kwa Agano la kale).
TOBA YA KWELI
Sote sisi tumejawa na dhambi. Toba ya kweli ni kukubali kufuata kweli; kwamba sisi ni wenye dhambi mbele ya Mungu, na hivyo hatuwezi kujizuia kutenda dhambi maishani mwetu na kwenda jehanamu tutakapokufa. Hivyo yatupasa kumkubali Yesu kama mwokozi wetu kwa kuamini kwamba alikuja ulimwenguni kutuokoa sisi wenye dhambi na hivyo alibeba dhambi zetu (kupitia ubatizo), akafa na alifufuliwa kutuokoa. Toba ya kweli ni kuacha fikra zetu na kumrudia Mungu (Matendo 2: 38).
Toba ya kweli ni kukiri dhambi zetu na kulirudia neno la Mungu kukubali wokovu katika maji (ubatizo) na kwa damu kwa moyo wetu wote. (1Yohana5:6).
Ili tuweze kuokolewa na kusafishwa dhambi zetu zote, yatupasa kuacha kujaribu kujitakasa kwa kupitia matendo ya sheria, na kukiri kwamba sisi ni wenye dhambi mbele ya Mungu na sheria yake, sisi basi yatupasa kukubali kweli ya wokovu wa Yesu, injili ya Maji na Roho, ambayo Yesu alituachia kwa ubatizo na damu yake.
Tutaokolewa pale tutakapo amini ubatizo wa Yesu uliozichukua dhambi zetu zote kwake.
Kwa maneno mengine, ubatizo wa Yesu, kusulubiwa kwake, na ufufuo wake umetimiza haki ya Mungu kwa wokovu wa wenye dhambi. Yesu alikuja katika mwili, alibatizwa na kusulubiwa ili kutusafisha dhambi zetu zote. Kwa kuwa na imani iliyo kamili katika yote haya na kuamini kwamba Yesu alifufuka ili awe mwokozi wa wote wenye kumwamini katika toba ya kweli na imani halisi.

Kila kitu katika Agano la kale kina mwenzake katika Agano jipya kwa Agano la kale “tafuteni katika kitabu cha BWANA mkasome hapana katika hao wote atakayekosa kuwapo, hapona mmoja atakayemkosa mwenzake; kwa maana kinywa change kimeamuru na roho yake imekusanya” (Isaya 34:16)
Hitimisho; ikiwa utajikuta wewe mwenyewe unamwomba Yesu ili akusamehe dhambi zako za kila siku, basi ni lazima utambue kuwa bado hujazaliwa upya.
Ikiwa kwa namna yoyote ile umekuwa ukijifanya kuwa mtakatifu kwa matendo yako na mwonekano wa mwili wako, ingawa moyo wako una dhambi, basi wewe ni mwanadini mnafiki na ni mtoto wa maangamizi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni